25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Makamu wa Rais awaweka njia panda walioshinda kura za maoni CCM

Na DERICK MILTON-SIMIYU

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema vikao vya juu vya maamuzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vitawasaidia wananchi kuwaletea viongozi bora na waadilifu kwenye maeneo ambako wameshinda ambao hawana sifa hizo.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu wakiwemo viongozi mbalimbali, kwenye hafla ya ufunguzi wa maonesho ya kilimo na sherehe za wakulima (Nanenane) kitaifa zilizofanyika viwanja vya Nyakabindi Mkoani humo.

“ Na kwa kuwa uchaguzi wa awali kwa chama cha mapinduzi umeishafanyika, pale ambapo mmeteleza kuwachagua viongozi bora na waadilifu, basi vikao vya juu vya chama vitawasaidia kutekeleza hilo, ili muweze kupata viongozi waliosahihi,” alisema Makamu wa Rais.

Akirejea kauli mbiu ya mwaka huu ya maonyesho hayo ambayo inasema kuwa; “kwa maendeleo ya kilimo, mifugo na Uvuvi chagua viongozi bora 2020” alisema kauli mbiu hiyo inaendana na kipindi tulichonacho.

Alisema kuwa kauli mbiu hiyo inatoa hamasa kwa wananchi kuhakikisha wanachagua viongozi bora 2020 watakaokuwa chachu ya kuleta mapinduzi katika sekta za uzalishaji na kuinua uchumi na ustawi wa wakulima, wafugaji na wavuvi.

“ Ili kuweza kutekeleza vema kauli mbiu hii, pale ambapo kwenye kura za maoni wameteleza, vikao vya juu vya chama vitahakikisha vinawaletea viongozi ambao wanaendana na kauli mbiu hiyo,” alisema Makamu wa Rais.

Aliwataka wananchi kutumia nafasi yao vema katika uchaguzi mkuu ujao, baada ya chama hicho kuwaletea viongozi bora na waadilifu wenye sifa zote za kuwa kiongozi kwa ajili ya kuwachagua.

“ Baada ya kuwaletea viongozi bora, niwatake wananchi mjitokeza kwa wingi kuhakikisha mnaenda kupiga kura na kuwapata viongozi bora ambao watakuwa wanatoka Chama Cha Mapinduzi,” aliongeza Makamu wa Rais.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Makamu wa Rais alipongeza wizara zote zinazohusika kwa kuendelea kuboresha mazingira mbalimbali ya wakulima, wafugaji na wavuvi ikiwemo kuongeza teknologia mpya za kuongeza tija.

“ Sekta ya kilimo nchini imeendelea kuwa mhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi wa taifa letu, katika kipindi cha miaka mitano pato la taifa litokanalo na kilimo kwa kutumia bei za mwaka 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka sh. Trilioni 25.2 hadi sh. Trilioni 29.5 mwaka 2019,” alisema Makamu wa Rais.

Aidha ameipongeza Wizara ya Kilimo kutokana na nchi kuwa na utoshelevu wa chakula kwa wastani wa asilimia 121 na kuwa na wastani wa ziada ya takribani tani milioni mbili.

Pamoja na hilo, Samia aliitaka Wizara ya kilimo kuhakikisha inawasimamia watafiti wake ambao wamefanya taifiti nyingi kwenye kilimo kuhakikisha majibu ya tafiti hizo yanawafikia walengwa.

“ Watafiti wanafanya kazi nzuri na kupata mbegu bora zinazokinzana na magonjwa pamoja na mbegu zinazohimili mabadiliko ya tabia nchi, hata hivyo matokeo ya tafiti zilizo nyingi hayawafikii walengwa.

“ Nitoe rai kwa watafiti wote nchini kutoa matokeo ya tafiti zenu kwa maofisa ugani na wadau wengine ili wakulima waweze kunufaika na matokeo hayo,” alisema.

Kuhusu sekta ya uvuvi, aliuagiza Wizara ya Uvuvi kuendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria, wale wote ambao wanaendeleza uvuvi haramu katika maziwa, mito na bahari.

Aidha alisema serikali itawachukulia hatua wale wote ambao wanaendelea kuendesha shughuli za kilimo katika vyanzo mbalimbali vya maji kwani wanaharibu mazingira.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema licha ya mikoa mingi kuzalisha mazao mbalimbali lakini bado imeendelea kuwa tatizo kubwa la watoto wenye udumavu wa akili.

Alisema inashangaza kuona mikoa ambayo inaongoza kwa kuzalisha mazao mengi ya chakula kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye udumavu, hali ambayo alisema juhudi zinahitaji katika kutoa elimu kwa wananchi.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa mkoa wa Njombe ndiyo kinara wa udumavu huo ukiwa na asilimia 53.6, ukifuatiwa na Rukwa asilimia 47.9, Iringa 41.7, Songwe 43.3, Kigoma 42.3 huku Ruvuma ambao ndiyo mkoa unaoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini ukiwa na asilimia 41.2 ya udumavu.

Alisema kutokana na hali hiyo Wizara hiyo imezundua mwongozo wa mafunzo ya lishe bora kwa wakulima, ikiwa ni moja ya hatua za serikali kwa kushirikiana na  shirika la mpango wa chakula duniani (WFP) katika kupamba na hali hiyo.

Aidha alisema mbali na kuzindua mwongozo huo, Wizara pia imezindua mwongozo wa kitaifa wa uongezaji wa virutubisho kibaiologia katika mazao ya chakula.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Simyu, Antony Mtaka, aliitaka wizara kuwekeza katika akili badala ya kuwekeza kwenye maonyesho hayo ili kuhakikisha wakulima wanazalisha kwa tija.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles