Faraja Masinde -Dar es salaam
JAMII imeaswa kuwalinda watoto kutojihusisha na kucheza kamari kutokana na kukithiri kwa matokeo hasi ya michezo hiyo.
Wito huo ulitolewa juzi Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini (GBT), James Mbalwe wakati akizindua kampeni ya ‘mlinde mtoto’ inayolenga kutokomeza vitendo vya kamari kwa watoto.
Alisema lengo la kampeni hiyo ni kuwalinda watoto, lakini pia ni kuihimiza jamii kutoa taarifa pale atakapoona mtoto anashiriki kamari bila kujali yuko na nani.
“Lengo la kampeni hii ni kuielimisha jamii juu ya katazo la kisheria la ushiriki wa watoto chini ya miaka 18 kwenye michezo ya kubahatisha ambayo haitakiwi.
“Na hatua hii tumeifikia baada ya kuwapo kwa kundi kubwa la wazazi ambao wamekuwa wakitupa malalamiko mengi kuhusu ushiriki wa watoto kwenye michezo ya kubahatisha.
“Bodi kwa kutambua kuwa watoto ni taifa la kesho hivyo tukaona ni lazima tuweke mkazo kwa ajili ya kuihimiza jamii ili kila mtu awe balozi kwa watoto wanaoshiriki kamari.
“Sisi hatuwezi kuwa kila mahali na ndiyo maana tunataka jamii kuwa mabalozi wetu kwani tumekuwa tukifanya hivi kila mwaka, mfano mwaka jana tulikuwa na kampeni inayosema ‘Ushiriki wa vijana katika kamali siyo ajira’ hivyo tuanendelea kufanya hivyo kulingana pia na malalamiko yanayoletwa na jamii, hivyo tunapaswa kushikamana,” alisema Mbalwe.
Alisema wazazi wanatakiwa kuwa makini ikiwa ni pamoja na kuangalia mienendo ya watoto wao ikiwamo kutokuwapatia simu ambazo wamekuwa wakizitumia kushiriki michezo ya kamari ili kuwa na taifa salama la kesho.
Aidha, mbali na uzinduzi wa kampeni hiyo, bodi hiyo pia ilitoa vifaa vya kusaidia kuzuia maambukizi dhidi corona kwenye maonyesho ya 44 ya Sabasaba Dar es Salaam ikiwa ni hatua ya kusaidiana na Serikali kutokomeza janga hilo.