AVELINE KITOMARY – DAR ES SALAAM
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa mara ya kwanza imefanikiwa kuokoa maisha ya watoto wawili waliozaliwa wakiwa na tatizo la tumbo wazi na utumbo kuwa nje (Gastroschisis).
Hatua hiyo imetokana na utaratibu wa kuwavalisha mifuko maalumu (Silo bags) ambayo haihusishi mtoto kufanyiwa upasuaji wala kupewa dawa za usingizi.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Daktari Bingwa Upasuaji wa Watoto, Zaitun Bokhary, alisema kabla ya kuwepo teknolojia hiyo, mtoto alikuwa akizaliwa na tatizo hilo uwezekana wa kupona ulikuwa haupo lakini kwa sasa uwezekano wa kupona ni asilimia 100.
“Kabla ya teknolojia hii kuwepo watoto wenye tatizo hili ilibidi wafanyiwe upasuaji na kuvalishwa mifuko ya kawaida ambayo ufanisi wake ulikuwa mdogo na ulihusisha kupitia taratibu mbalimbali za upasuaji ikiwemo kupewa dawa za usingizi ambapo kutokana na uchanga wa watoto na muda ulikuwa unatumika kurejesha matumbo, watoto walipata madhara ikiwemo vifo.
“Kuanzia sasa mtoto akizaliwa na tatizo hili atavalishwa mfuko maalumu unaotunza majimaji akiwa wodini ambapo kila siku watoa huduma watakua wanausukuma utumbo kurudi tumboni kwa vipimo maalumu na katika kipindi cha siku tatu hadi tano, utumbo utakuwa umerudi kwenye hali ya kawaida, baada ya hapo mtoto atafungwa tumbo kwa njia maalumu ambayo haiusishi kushonwa na nyuzi,”alibainisha Dk Bokhary.
Alieleza ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana katika maeneo mengi nchini, jukumu la kutoa mafunkzo maalum limeanza.
“Hospitali ya Taifa Muhimbili imechukua hatua ya kutoa mafunzo maalumu kwa hospitali zote za kanda zilizopo Mkoa wa Dar es salaam juu ya namna ya kuwapa huduma ya kwanza watoto wanaozaliwa na na tatizo hili kabla ya kuwapa rufaa ya kufika Muhimbili ambapo kwa sasa ndio sehemu pekee utaalamu huu unapatikana,”alisema
Aliongeza kuwa MNH itaendelea kutoa mafunzo hayo kwa hospitali zingine nchini.