MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
IDADI ya wagonjwa walioambukizwa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid 19), imeongezeka na kufikia 147 baada ya wengine wapya 53 kukutwa na ugonjwa huo.
Idadi hiyo maana yake kuna ongezeko la wagonjwa 115 ndani ya wiki moja, kwani hadi kufikia Ijumaa iliyopita kulikuwa na wagonjwa 32 tu waliokuwa wameambukizwa virusi hivyo.
Akitangaza idadi hiyo mpya jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kati ya wagonjwa hao wapya 53, 38 ni kutoka Dar es Salaam, 10 kutoka Zanzibar, Mwanza 1, Kagera 1, Lindi 1, Kilimanjaro 1 na Pwani 1.
“Katika upimaji wa sampuli ambayo tumepima katika maabara za taifa ya afya ya jamii jana (juzi) Aprili 16 na leo (jana) Aprili 17 zinaonyesha kuwepo watu 53 wapya wenye maambukizi ya corona wote ni Watanzania na 38 wako Dar es Salaam, 10 Zanzibar, Mwanza 1, Kilimanjaro 1, Lindi 1, Pwani 1 na Kagera 1.
“Lakini pia tunasikitika kutangaza kifo cha mgonjwa mmoja wa corona. Hivyo sasa idadi ya wagonjwa imefika 147 tangu tulipotangaza mgonjwa wetu wa kwanza Machi 16 mwaka huu na waliopona ni 11, waliofariki ni watano, wote waliobaki hali zao ni nzuri isipokuwa wagonjwa wanne tu ambao hali zao ni mbaya.
“Kati ya wagonjwa 131 wanaobaki, wagonjwa 127 hali zao ni nzuri wanatembea wengine wanafanya mazoezi wanapiga push up, tumewazuia katika vituo vyetu vya matibabu kwa sababu tukiwapima majibu bado ni positive na hatuwezi kuwaruhusu watoke.
“Niwatoe hofu Watanzania walioambukizwa kasoro wanne wanaendelea vizuri,”alisema Ummy.
WHO YAONYA
Wakati huo huo Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa onyo jingine likisema Afrika inaweza kuwa kitovu kinachofuata cha mlipuko wa virusi vya corona.
WHO limetoa onyo hilo kutokana na kile ilichosema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la visa vya watu wanaokufa na kuambukizwa virusi hivyo katika kipindi cha wiki moja.
Kumekuwa na vifo vya karibu 1,000 na zaidi ya maambukizi 18,000 katika bara zima la Afrika hadi sasa, ingawa viwango hivi ni vya chini sana ukilinganisha na vile vinavyotokea katika Bara la Ulaya na Amerika.
Takribani mwezi mmoja uliopita WHO lilitahadharisha jambo linalofanana na hilo likisema Afrika licha ya kuwa bara lililoathirika kwa kiwango cha chini likilinganishwa na mabara mengine, lakini mifumo duni ya afya ya umma inaweza kuzidiwa uwezo haraka na hivyo kujikuta na maambukizi mengi ndani ya muda mfupi.
WHO limesema kuwa virusi vya corona sasa ni dhahiri vinaonekana kuenea katika miji mikubwa mingi ya Afrika.
Pia WHO limedokeza kuwa bara hilo halina mashine za kutosha za kusaidia kupumua (ventilators) ili kupambana na ugonjwa huo.
KUENEA KWA VIRUSI VYA CORONA KUNAVYOIJARIBU AFRIKA
Mkuu wa WHO katika kanda ya Afrika, Dk. Matshidiso Moeti, ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kwamba shirika hilo limeshuhudia virusi hivyo vikienea kutoka miji mikubwa kwenda katika miji ya jirani nchini Afrika Kusini, Nigeria, Ivory Coast, Cameroon na Ghana.
Alisema wamejikita zaidi kwenye kuzuia kuliko kutibu virusi hivyo kwa sababu nchi za kiafrika hazina uwezo wa kutibu wagonjwa wa virusi vya corona.
“Tunataka kupunguza idadi ya watu wanaoweza kufikia hatua ya kuhitaji uangalizi maalumu katika ICU, kwa sababu tunafahamu kwamba vifaa havipo vya kutosha katika nchi nyingi za Afrika,” alisema.
“Ninaweza kusema vifaa kama vya kusaidia kupumua (ventilators) ni changamoto kubwa zinazokabili nchi nyingi.”
Kwa wagonjwa wa virusi vya corona ambao wako katika hali mbaya kutokuwa na huduma ya vifaa vya kuwasaidia kupumua ni suala la maisha na kifo.
Mashine hizo husaidia kupeleka hewa ya oksijeni kwenye mapafu na kutoa ile ya carbon dioxide kutoka kwenye mwili wakati ambao mtu anakuwa anaumwa sana kiasi cha kushindwa kupumua sawasawa.
Kuna hofu kwamba ugonjwa huo unaweza kuenea kwa kasi kubwa kwenye maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ambako ni vigumu kutotengemana na watu ‘social distancing” na mahali ambako wengi ni vigumu kupata huduma ya maji safi na sabuni.
WAZIRI UMMY
Awali Jana asubuhi wakati akizindua mwongozo wa mpango wa huduma za afya katika jamii na matumizi ya dashibodi ya viashiria vya elimu ya afya kwa umma, Ummy aliwataka Watanzania kutumia namba za simu zilizotolewa kutoa taarifa sahihi za wanaohisi wana dalili za ugonjwa ili wapatiwe matibabu na sio kufanya mchezo.
“Sio unanipigia simu mimi unaniambia una corona halafu napigia Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuwa nimepokea taarifa kuna mtu anasema ana corona katika eneo hilo, halafu RC anaamka na simu yake wanaendesha magari zaidi ya kilomita 100 kwenda kumtafuta huyo mtu halafu wanafika pale amezima simu, akaamua kupotea na akawasha siku ya pili mchana.
“Katika hili naomba sana tutumie namba za simu tunazozitoa pamoja na namba yangu kwa ajili ya kutoa taarifa sahihi kwa ajili ya kupata huduma na sio kufanya mchezo,”alionya Ummy.
Akizungumzia mwongozo huo, Ummy alisema Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika kuimarisha huduma za kinga, ikiwemo elimu ya afya na uhamasishaji, lishe, udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na afya ya mama na mtoto.
“Hii itasaidia juhudi za kupunguza mzigo wa gharama za matibabu unaowatesa wananchi na kuongeza matumizi ya serikali katika tiba ya magonjwa yanayoweza kuzuilika au kuepukwa,” alisema Ummy.
Mkakati huo wa kutumia watoa huduma za afya kwa jamii utawezesha kuwepo kwa huduma imara za kinga katika ngazi zote ikiwemo utoaji elimu ya afya na uhamasishaji kama njia muhimu ya kusaidia jamii kujikinga na magonjwa.
Kutokana na hali hiyo alisema serikali inatambua kuwa jamii yenye elimu sahihi juu ya vyanzo vya afya bora na masuala yanayoweza kuathiri afya hufanya maamuzi sahihi juu ya mambo yanayohusu afya zao.
“Hii itawezesha Taifa letu kuwa na wananchi wenye afya njema wanaochangia katika maendeleo yao, familia zao, jamii wanayoishi na nchi yetu kwa ujumla,” alisema
Waziri Ummy alisema serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya ili kufikia malengo ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote yaani Universal Health Coverage ambavyo itajumuisha utoaji elimu ya afya juu ya mambo yahusuyo lishe, afya ya uzazi, watoto na vijana ikijumuisha magonjwa ya mlipuko kama COVID-19 pamoja na magonjwa yasiyoambukiza.
“Hata hivyo sambamba na takwimu za wagonjwa, pia tumeshuhudia ongezeko la vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza hadi kufikia asilimia 33 ya vifo vyote nchini kwa mwaka 2017, ambapo jumla ya vifo 134,600 viliripotiwa na kuhusishwa na magonjwa yasiyoambukiza” alisema.
“Huku vifo vitokanavyo na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu vikichangia kwa asilimia 13, idadi ambayo ni kubwa kuliko ile itokanayo na magonjwa kama Ukimwi, Kifua Kikuu au Malaria,”.
Waziri Ummy, alisema matatizo yote hayo yanaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa endapo wataimarisha mifumo ya kutoa elimu na taarifa sahihi kwa jamii juu ya namna ya kuepuka kwa kufuata kanuni bora za afya pamoja na kuwatumia vyema wahudumu afya za jamii kuanzia ngazi za kijiji na mtaa.
“Pia Wahudumu wa afya ya jamii hawa waende wakahamashishe jamii zetu kujenga desturi ya kutafuta huduma rasmi za afya ikiwa ni pamoja na kujiunga kwenye mifuko yetu ya bima za afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya,” alisisitiza.