26 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Hukumu ya akina Mbowe kutolewa leo

Kulwa Mzee -Dar es salaam

HAKIMU Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Thomas Simba, leo anatarajia kusoma hukumu dhidi ya vigogo wa Chadema akiwemo, Mwqenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, akiwa ametumia siku 361 kusikiliza kesi hiyo hadi kufikia hukumu.

Mahakama inafikia hatua hiyo baada ya miaka miwili ya kesi hiyo kufika katika Mahakama ya Kisutu na mwaka mmoja kasoro siku nne kwa Hakimu Simba kupokea jalada na kuanza kusikiliza upya kesi hadi kufikia mwisho.

Kina Mbowe wanatarajia kusomewa hukumu baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili.

Awali kesi hiyo ilipoanza Machi mwaka 2018 ilikuwa inasikilizwa na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ambaye aliteuliwa kuwa Jaji Machi mwaka jana na jalada la kesi hiyo kuhamia kwa Hakimu Simba Machi 14 mwaka huo.

Kwanini Hakimu Simba katumia muda mfupi kumaliza kesi? Alipokea jalada la kesi hiyo Machi 14 mwaka jana na aliamuru washtakiwa wasomewe upya mashtaka 13 yanayowakabili.

Wakati akianza kusikiliza kesi, alitoa mwongozo kwa mawakili wa pande zote mbili na kuweka misimamo yake, akionyesha kipi hapendi kukiona wakati kesi ikiendelea.

Hakimu Simba aliwaambia mawakili kwamba hataki mapambano yanayosababisha mahakama kufikia hatua ya kutoa uamuzi mdogo, alikataa mabishano yasiyokuwa ya msingi yenye lengo la kuchelewesha kesi.

Hakimu alikataa ruhusa zisizo za msingi kwa washtakiwa na katika mwaka huo mmoja alitumia zaidi maonyo kwa washtakiwa bila kuwapeleka mahabusu kwa kuruka dhamana kama ambavyo Jamhuri waliomba baadhi wafutiwe dhamana.

Aliepuka kuwafutia dhamana washtakiwa akisema hatua hiyo ni hatua kali sana, hivyo aliwaonya na kuonyesha kwamba baadhi ya sababu zao hazikuwa na msingi.

Februari 24 mwaka huu, Hakimu Simba alisema hukumu itasomwa leo. Upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi 13 hadi wanafunga ushahidi na upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi nane.

Alisema tarehe ya hukumu ni Machi 10 mwaka huu saa nne na nusu asubuhi.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi ulifunga ushahidii wakiwa na jumla ya mashahidi nane.

Kesi hiyo ilipoanza mbele ya aliyekuwa Hakimu Wilbard Mashauri ilikuwa na mvutano wa kisheria wa mara kwa mara na Novemba 23 mwaka juzi Mshtakiwa Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko walijikuta wakienda gerezani kwa miezi mitatu kwa kosa la kutohudhuria mahakamani wakati kesi inaendelea.

Mbowe na Matiko walipata baraka za Mahakama Kuu mbele ya Jaji Sam Rumanyika ambaye alitengua uamuzi huo Machi 7 mwaka jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles