Na Derick Milton, Simiyu.
Serikali imempongeza mwekezaji wa kiwanda cha kuchambua pamba Alliance Ginnery kilichopo Wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu kwa kujenga chuo cha ufundi kisha kukibadhi serikali.
Kiwanda hicho kilichopo katika kijiji cha Kasori Wilayani humo, kimeweza kujenga chuo hicho kwenye kijiji hicho ambacho kitakuwa na kozi za ufundi selemala, uchomeleaji, fundi mwashi, hotel, pamoja na ushonaji.
Akiweka jiwe la Msingi ujenzi wa chuo hicho Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga alimpongeza mwekezaji huyo, huku akibainisha kuwa ni jambo la kipekee mwekezaji kujenga chuo kisha kukikabidhi serikali.
” Ni wawekezaji wachache sana wanaoweza kufanya hivi, alikuwa na uwezo wa kujenga na kukiendesha mwenyewe na kuwatoza wananchi wanaotaka kuleta vijana wao wapate ujuzi, lakini huyu katoa bure kwa wananchi na serikali iweze kukisimamia” Alisema Kiswaga.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa chuo hicho Mtendaji wa kata ya Kasori Gindu Ntemi alisema kuwa hadi kukamilika kwake chuo hicho kitagharimu kiasi cha sh.180 ambapo mwekezaji huyo amenunua pia pamoja na vifaa vya kutumika katika ufundishaji ikiwemo vyerehani.
Diwani wa Kata hiyo Mayala Lucas alisema kuwa mwekezaji huyo ameebdelea kuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa kata hiyo kwani ametumia zaidi ya sh.Milioni 800 kuwasaidia katika huduma mbalimbali za kijamii.
Lucas alisema kuwa chuo hicho kinaenda kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwani wengi wao wanahitimi kidato cha nne na darasa la saba lakini hawana sehemu ya kujipatia ujuzi.