KHARTOUM,SUDAN
MAZUNGUMZO ya kutatua masuala yaliyobaki kati ya waandamanaji wa Sudan na watawala wa kijeshi yanatarajiwa kuanza leo.
Hayo yanajiri wakati waandamanaji kadhaa wakimiminika mitaani mjini Khartoum kuitisha uchugunzi huru kuhusiana na ukandamizaji mkubwa uliofanywa dhidi ya kambi ya maandamano mwezi Juni.
Pande hizo mbili tayari zimesaini makubaliano ya kugawana madaraka ambayo yanalenga kuunda baraza tawala la pamoja la kijeshi na kiraia ambalo litapisha utawala wa kiraia.
Mpatanishi wa Umoja wa Afrika, Mohamed El Hacen Lebatt, amesema katika taarifa kuwa pande zote mbili zimealikwa kushiriki mazungumzo ya mwisho kuhusu tamko la kikatiba.
Mazungumzo hayo yatahusu masuala kama vile mamlaka ya baraza tawala litakaloundwa, kutumika kwa vikosi vya usalama na kinga ya majenerali kutokana na machafuko yanayohusiana na maandamano.