Bakari Kimwanga -Dar es Salaam
KAMISHNA wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Freddy Manongi, amesema kuna mafanikio katika kupambana na ujangili kwani katika kipindi cha miaka minne hakuna tembo wala faru aliyeuawa na majangili.
Manongi alisema hayo jana Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza kwenye programu maalumu kwa waandishi wa habari kutoka Thailand na Tanzania, iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa USAID-Protect.
“Hili kwetu tunajivunia sana kwani katika miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli kwa kweli hakuna mzoga wa tembo ambao nimeukuta katika eneo la mamlaka au hata kuripotiwa kwenye hiafadhi nyingine nchini kwamba kuna mnyama kauawa na majangili.
“Hata ukiona tembo amekufa basi ni kwa mambo mengine, lakini si ujangili. Hivyo imefanya kuongezeka wanyama wetu jambo ambalo ni la kujivunia,” alisema Dk. Manongi.
Pamoja na hali hiyo, alisema licha ya juhudi zinazochukuliwa na Serikali, bado jamii inatakiwa kunufaika na mapato yatokanayo na hifadhi.
Alisema pamoja na Mamlaka ya Ngorongoro kupata mafanikio, mwaka 2017 kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), walifanya sensa ya watu na wanyama ambapo ilibainika changamoto kadhaa ikiwamo ongezeko la shughuli za watu zaidi ya 95,000 katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
“Idadi ya watu imeongezeka na hili linatokana na mila zinazochangia shughuli za binadamu. Lakini pia idadi ya mifugo inaongezeka hali ambayo imesababisha kuwapo kwa magonjwa toka kwa wanyama kwenda kwa binadamu ikiwamo kimeta na minyoo.
“Sensa hii pia ilibanika zaidi ya asilimia 60 ya watu wanaoishi ndani ya hifadhi hawajui kusoma na kuandika. Sasa hii ni changamoto, sisi kama mamlaka tumejenga shule 21 za msingi na za sekondari mbili ambazo zina kidato cha tano na sita.
“Pia Serikali imekuwa ikitoa kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya kugharamia elimu, swala ambalo nasi tunajiuliza je, mfumo wetu na walimu hawana maarifa ya kutosha au nini? Hili ni swali ambalo bado linatuumiza vichwa sana,” alisema Dk. Manongi.
Alisema pamoja na hali hiyo bado mamlaka yao imekuwa ikifanya vizuri kwa upande wa mapato ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 walikusanya Sh bilioni 120 na kupokea wageni wa ndani na nje ya nchi 600,000.