- Msigwa agoma kuisoma, Mambo ya Ndani yamwaga ajira za Polisi
MAREGESI PAUL-DODOMA
HOTUBA ya Bajeti ya Wazira ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kwa mwaka 2019/20, imezua jambo bungeni baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kugoma kusoma maoni yao kwa mara ya pili mfululizo kutokana na kile walichodai ilikuwa imehaririwa.
Aprili 18, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi aligoma kusoma maoni ya kambi hiyo kuhusiana na Hotuba ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, kwa madai kama hayo.
Walisema hotuba waliyopeleka ofisi ya bunge kwa ajili ya kuchapishwa ilihaririwa na kuwa tofauti na maoni yao.
Jana, baada ya Lugola kusoma hotuba yake, Msemaji wa upinzani kwenye wizara hiyo, Mchungaji Peter Msigwa, alitakiwa kusoma maoni ya kambi yao.
Mchungaji Msigwa aligoma kusoma hotuba yake kwa kile alichosema ilikuwa imehaririwa na kuondolewa baadhi ya maneno waliyotaka kuyafikisha kwa wananchi.
Dalili za kambi hiyo kutosoma hotuba yake zilianza mapema baada Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema), kusimama na kuomba kuhusu utaratibu, muda mfupi baada ya Lugola kuwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake.
Katika maelezo yake, Matiko alimwambia Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, kwamba hotuba yao ilikuwa imehaririwa na kuondolewa baadhi ya maneno muhimu, jambo ambalo alisema liliondoa uhalali wa wao kuitwa kambi ya upinzani.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, jana (juzi), tulipeleka hotuba yetu ikachapishwe kule, lakini baada ya kuchapishwa, imefanyiwa ‘editing’ kwa kuondolewa mambo mengi.
“Kwa kweli hii siyo haki, hayo mnayoondoa ndiyo maoni yetu, sasa mtayaondoaje?
“Mheshimiwa mwenyekiti, wewe ni mwanasheria mzoefu, hebu tueleze kuhusu huu utaratibu, nawaomba msiogope kivuli chenu.
“Kwa hiyo, mheshimiwa mwenyekiti, tafadhalini mrudishe maneno mliyoondoa hotuba yetu iweze kusomwa kwa ukamilifu wake,” alilalamika Matiko.
Akijibu kuhusu utaratibu, Chenge alisema hajaona mahali popote kanuni zilipovunjwa na kusema uamuzi wake ni Kambi ya Upinzani kusoma hotuba mpya waliyogawiwa wabunge wote na siyo hotuba waliyonayo,” alisema Chenge.
Baada ya mvutano huo, ilipofika zamu ya Mchungaji Msigwa kuwasilisha maoni ya kambi yake, Chenge alimtahadharisha akimtaka asome hotuba mpya isiyokuwa na maneno yasiyokubalika.
Pamoja na maelekezo hayo, Mchungaji Msigwa alipoanza kusoma hotuba yake, hakuruka maneno yaliyotakiwa kurukwa, hivyo Chenge akalazimika kumsimamisha kwa kumtaka afuate maelekezo yake.
“Mheshimiwa Msigwa, nimeshasema kwamba hotuba zitakazosomwa hapa ni ile ya Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama pamoja na ile ya upinzani iliyogawiwa kwa wabunge.
“Nakwambia soma hotuba iliyoruhusiwa na siko tayari kuruhusu hotuba nyingine zaidi ya hiyo, isomwe hapa,” alionya Chenge.
Baada ya maelekezo hayo, Mchungaji Msigwa alilalamika na kusema asingeweza kusoma hotuba nyingine tofauti na iliyoandaliwa na kambi yake.
“Siko tayari kusoma hotuba nyingine zaidi ya hii kwa sababu hayo unayotaka tusome ni maoni ya Serikali siyo ya upinzani.
“Mheshimiwa mwenyekiti, what are we doing, tumekuja kufanya nini hapa?
“Mimi ni mpinzani na walionileta hapa wanajua nimekuja kuwawakilisha, kwa hiyo, nikisoma maoni ya Serikali nitakuwa siwatendei haki walionileta hapa,” alisema Mchungaji Msigwa huku akielekea kukaa.
Kwa sababu hiyo, Mwenyekiti Chenge aliruhusu mjadala wa hotuba hiyo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi uanze na wabunge walianza kuchangia.
Wiki iliyopita, Sugu aligoma kusoma hotuba yake mbele ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, ambaye ndiye aliyekuwa akiongoza kikao cha siku hiyo.
Sugu alisema asingeweza kusoma hotuba ambayo ilikuwa ni tofauti na iliyoandaliwa na kambi yake.
Pamoja na msimamo wa mbunge huyo, Dk. Tulia alimtaka Sugu asome hotuba mpya waliyokuwa wamegawiwa wabunge badala ya hotuba aliyokuwa nayo mkononi.
Kutokana na mvutano huo, Sugu aliamua kuacha kusoma hotuba hiyo na kumfanya Naibu Spika aruhusu shughuli nyingine za Bunge ziendelee.