Mwandishi wetu, Dodoma
Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga, amesema hajawahi kuingia bungeni akiwa amelewa na hilo halitakaa litokee.
Kitwanga amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa 2019/20.
Wakati akichangia mpango huo, Kitwanga alisema ukiimarisha Shirika la Ndege la Taifa, utalii utakua kwasababu watalii wakifika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, watachukuliwa na ndege nyingine hadi Mwanza ambapo atachukuliwa na gari la mti wa Kolomoje na kupelekwa mbuga za wanyama.
“Wasiojua hili ni watu wa upande huu,” alisema huku akimaanisha wapinzani.
Baada ya kusema hivyo upande wa upinzani walianza kuzomea na wengine wakiomba kutoa taarifa, Kitwanga alisema “kwani nimesema upande gani, nimesema upande huu.”
Spika Job Ndugai, aliyekuwa akiongoza kikao hicho aliwakatalia waliokuwa wakiomba taarifa na kusema; “vumilieni haya ni mambo madago, yaani ukitekenywa tu unatekenyeka.”
Kitwanga aliendelea kuchangia na kusema kuwa, kuna kampuni za kitanzania zinajenga barabara ikiwamo inayojenga barabara ya Ubungo, Kibaha akisema fedha watakazolipwa zitabaki nyumbani.
“Kwa hiyo niwaombe ndugu zangu mliokaa huku mbele, mlitambue hilo mshirikiane na mimi nilikuwa nikikaa mwanzoni ninyi nyote ni wenzangu, na mimi nirudie tena kusema Mtanzania anayependa nchi yake ataitumikia nchi yake mahala popote.
“Let me say this thing once and for all, I have never being in this house drank, I will not do that, and it will never happen, (ngoja niseme hili jambo kwa mara nyingine tena, sijawahi kuwa ndani ya ukumbi wa Bunge nikiwa nimelewa, siwezi kufanya hivyo na haitakuja kutokea) mnaoendelea kusema hivyo, endeleeni na mtaendelea hadi Yesu atakapokuja,” amesema Kitwanga.
Kauli hiyo ilifanya wabunge waangue kicheko huku wengine wakizomea hali iliyofanya Spika Ndugai kusema; “mnajua shida yetu hapa watu wengi hatufahamiani, mheshimiwa Kitwanga siyo mtu mwepesi, kabisa, yuko vizuri.”
Kitwanga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alitumbuliwa baada ya kudaiwa kuingia bungeni akiwa amelewa na kushindwa kujibu vyema maswali ya wabunge.