Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaac Kamwelwe, ameendelea kuwa katika wakati mgumu baada ya Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bungara (Bwege), kudai waziri huyo anamdharau Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Amesema Waziri Kamwelwe alitembelea jimboni kwake na kumueleza miradi ambayo Waziri Mkuu ameiridhia na Kamwelwe kutoa kauli iliyoonyesha ni kumdharau Waziri Mkuu.
Bwege ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 8, bungeni jijini Dodoma wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2019/20, ambapo pia amesema alidhani ni yeye pekee aliyejibiwa vibaya lakini alishangaa jana kumsikia Mbunge wa Mafia, Mbaraka Dau(CCM), akitoa maelezo kama yake.
“Dau alisema kitu kilichonisikitisha sana, Waziri Mkuu anachaguliwa na Rais na anathibitishwa na Bunge, jana hapa Dau alimwambia waziri habari ya boti, lakini akajibiwa majibu mabaya na Waziri wa Ujenzi, si mara moja hii, kuna mradi wa maji (Jimbo la Kilwa) nikamwambia naye akanijibu Waziri Mkuu nani, mimi namtambua Rais John Magufuli tu.
“Kuna mtu mmoja anamdhalilisha (Waziri Mkuu) si desturi nzuri waheshimiwa, huyu ni Waziri Mkuu asidharauliwe, sisi tukisema sana tunaitwa katika maadili,” amesema Bwege.
Baada ya kauli hiyo, Spika Job Ndugai, aliyekuwa akiongoza kikao hicho alisema “Bungara uko katika shughuli yako ya uchonganishi wako ili watu wagombane humu.”
Akijibu kauli hiyo, Bwege alisema; “Mheshimiwa Spika mimi nanukuu yaliyosemwa hapa jana.”
Katika kikao cha jana, Dau alidai Waziri Kamwelwe amekiuka agizo la Waziri Mkuu la kupeleka Mafia meli iliyotolewa na mfanyabiashara Said Salim Bakhresa, akidai ni maagizo ya kisiasa na kwamba suala la kupeleka meli hiyo Mafia walilijadili na Waziri Mkuu na akakubali ipelekwe Mafia jambo ambalo hata Profesa Makame Mbarawa aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, aliliridhia.