Na MWANDISHI WETU-MOROGORO
SERIKALI kupitia wizara zake zimeshauriwa kuhakikisha inatenga bajeti zenye mrengo wa jinsia ili kufikia lengo la kuwa na uchumi wa kati utakaowashirikisha wanawake na wanaume.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa wanawake Tanzania, Profesa Ruth Meena alikuwa akizungumza kwenye kikao kazi cha wakurugenzi wa mipango na sera kutoka wizara mbalimbali kilichoandaliwa na TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA).
Alisema Serikali inapaswa kuhakikisha kila bajeti inazingatia usawa wa jinsia kwa kuwapa kipaumbele wanawake kama ilivyo kwa wanaume.
Alisema bajeti inayozingatia usawa huo ndiyo njia mojawapo itayoiwezesha nchi kufikia kafikia malengo ya mkakati ikiwamo ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 -2025 unanyanyasaji wowote wa jinsia umekuwa umetoweka.
Profesa Meena alisema lengo ilkiwa ni kuondoa ubaguzi hususan kwa wanawake kama sehemu ya kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Jinsia kwa Wanawake na Watoto (NPA) ifikapo 2022.
“Kwa kiupindi cha zaidi ya miaka 25, TGNP tumesimamia eneo la bajeti ya mrengo wa jinsia, leo (juzi) siyo mara ya kwanza kukaa na watu wa serikali.
“Tunakutana na watendaji wa serikali kwa ngazi tofauti hadi makatibu wakuu, kuhakikisha wanaelewa masuala ya jinsia na kuyazingatia wakati wa kuandaa mipango yao na sera za nchi.
“Ni lazima pia jamii kutambua masuala ya jinsia ni uwiano sawa kati ya mwanamke na mwanamume katika nyanja zote,’’ alisema Profesa Meena
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi alisema baada ya kugundua baadhi ya wizara bajeti zake zilikuwa hazilengi moja kwa moja usawa wa jinsia, TGNP imeweza kukutana na wakurugenzi wa wizara mbalimbali kujadili umuhimu wa kupanga bajeti kwa kuzingatia usawa wa jinsia.
“Endapo serikali italiwekea mkazo zaidi suala hili la usawa wa jinsia katika bajeti zake nitasaidia kuongeza uwajibikaji na matumizi mazuri za rasilimali za nchi kwa sababu mwanamke atakuwa amehusishwa moja kwa moja katika bajeti hiyo bila kubaguliwa,” alisema Liundi.
Akifungua rkikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Jinsia sehemu ya wanawake kutoka Wizara ya afya ,Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mboni Mgaza alisema wizara imepewa jukumu la sera la kuratibu masuala ya usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake.
TGNP Mtandao kwa kushirikiana Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Shirika la Idadi ya watu Duniani (UNFPA) wanatekeleza kwa pamoja mradi wa kuhakikisha serikali kuu na serikali za mitaa zinatenga fedha kwenye bajeti yake kwa ajili ya kuwezesha kutokomeza mila potofu na vitendo vya ukatili wa jinsia nchini.