24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Wingu zito latanda kigogo UDART

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

Wingu  zito bado limetanda kuhusu wafanyakazi wanane  wa Kampuni ya Kampuni ya Kampuni ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) akiwamo kigogo wa Idara wa Fedha wa kampuni hiyo ambako hadi sasa Jeshi la Polisi limekataa  kueleza kama wanaendelea kushikiliwa au laa.

Wafanyakazi hao walikamatwa wakidaiwa kufyatua tiketi feki za mwendokasi na kusababisha hasara kwa serikali baada ya uchunguzi wa MTANZANIA kubaini madudu hayo   Juni mwaka huu.

MTANZANIA ilimtafuka Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, ambaye alisema kwa sasa yupo likizo na anayetakiwa kuzungumzia suala hilo ni aliyemuachia ofisi, Kaimu Kamanda Liberatus Sabas.

Gazeti hili lilimtafuta kwa zaidi ya siku tano Kaimu Kamanda Sabas bila mafanikio.

Hata hivyo  Alhamisi ya wiki iliyopita alipatikana na kusema kwamba kwa sasa hawezi kusema jambo lolote kuhusu watu hao na kama kuna suala zito atatoa taarifa kwa kuzungumza  na  wanahabari na si vinginevyo.

Licha ya majibu hayo,  alipoulizwa kama Jeshi la Polisi linaendelea kuwashikilia na ni lini watawafikishwa mahakamani, alisema   hawezi kuzungumzia suala hilo na kukata simu.

“Siwezi kusema jambo hili kwa sasa, ninatoka kwenye kongamano Chuo Kikuu ambako Rais Magufuli alishiriki, hivyo kama kuna jambo nitatoa ufafanuzi kupitia mkutano wa wanahabari wote,” alisema  na kukata simu.

Kaimu Kamanda huyo alitafutwa kutokana na matamshi ya  awali ya Kamanda Mambosasa   kwamba watumishi wanashikiliwa kwa kuisababisha serikali hasara ya mamilioni ya fedha.

Taarifa za ndani zilieleza kwamba jalada ya uchunguzi la wafanyakazi hao  akiwamo kigogo huyo wa idara ya fedha, lilipelekwa kwa DPP kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Wiki iliyopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, alisema wameanza mchakato wa mikataba wa kumtafuta mwekezaji wa pili wa  kutoa huduma ya mabasi ya mwendokasi   Dar es Salaam.

Alisema lengo ni kuongeza mabasi  kuondoa msongamano wa abiria uliopo sasa.

Mradi huo ambao Jafo alisema kwa sasa unahudumia abiria 350,000 kwa siku,  unaendeshwa na mwekezaji ambaye ni UDART kwa usimamizi wa DART.

Jafo alisema hatua hiyo inatokana na mwekezaji aliyepo kushindwa kufikia lengo la kuwa na mabasi ya kutosha yaliyokusudiwa katika mradi huo.

“Tulipoanzisha ule mradi lengo ilikuwa ni kuwa na mabasi 350 katika awamu ya kwanza, lakini UDART alinunua mabasi 140.

“Hadi sasa na abiria wameendelea kuongezeka kutoka 70,000 hadi 350,000 kwa siku hivyo tunataka yawepo mabasi mengi kadiri muda unavyokwenda.

“Sasa tupo kwenye mchakato wa mikataba kutafuta mwekezaji wa pili na tenda hiyo itatangazwa kimataifa ili kampuni kubwa zikiwamo za kimataifa ziweze kuja kuwekeza angalau tuweze kuwa na mabasi 350 kwenye awamu hii ya kwanza ya miradi ya mwendo kasi,” alisema.

Akizungumzia kuhusu dosari iliyojitokeza siku za karibuni katika mradi huo, alisema ilitokana na kosa la mwendeshaji ambaye ni UDART baada ya kuchelewa kulipa mishahara ya wafanyakazi wake hali iliyosababisha wagome.

“Matatizo kama haya yanapotokea wananchi wanairushia serikali lawama na kusema serikali imeshindwa kuendesha mradi kumbe tatizo ni kwa mwekezaji na si serikali,” alisema Jafo.

Hata hivyo alitoa wito kwa wananchi kuwa wavumilivu linapotokea tatizo katika mradi huo kwa sababu ni mradi mpya ambao unahitaji kujifunza na kuboreshwa siku hadi siku.

“Tunajifunza kutokana na makosa hivyo tunaendelea kuboresha   panapokuwa na dosari hivyo miradi inayokuja tunatarajia kusiwapo   changamoto hizo kwa vile  tumeshajifunza kwenye awamu ya kwanza,” aliongeza.

Alisema mradi unaofuata ni wa   kwenda Mbagala ukifuatia na ule wa mjini kwenda Gongo la Mboto, ambazo zinatarajiwa kumaliza tatizo la msongamano katikati ya jiji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,074FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles