Na AVELINE KITOMARY DAR ES SALAA
MADEREVA wa malori ya kusafirisha mafuta wanaoegesha magari yao Keko Mwanga B Dar es salaam, wameilalamikia Manispaa ya Temeke kuwatoza ushuru mkubwa wakati mazingira hayo hayana usalama na huduma sahihi kwa ajili ya maegesho.
Wakizungumza na MTANZANIA, madereva hao waliiomba manispaa hiyo kutenga eneo maalum kwa ajili ya maegesho ya magari na kuwawekea mazingira salama na utaratibu sahihi wa ulinzi ili walipe ushuru halali.
“Manispaa inatutoza Sh 2,000 kwa ajili ya maegesho ya magari huku hawajaweka mazingira sahihi ya kuegesha magari.
“Hapa ni barabarani si maegesho hivyo sisi madereva ndiyo tunaoumia.
“Fedha za ushuru hazitoki kwa mabosi wetu tunalipa wenyewe na ukikataa kulipa gari linafungwa minyororo.
“Tunataka manispaa itutengee maeneo maalum kwa ajili ya maegesho ya magari, hapa usalama ni mdogo pia hakuna huduma muhimu na utaratibu unaoeleweka,” alisema Sadick Masoud.