Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Mambo ya Nje wa Chama cha Wananchi (CUF- upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad), Ismail Jussa, amesema hivi sasa vyama vya upinzani vinavurugwa lakini utafika muda vitaungana na kutengeneza taasisi imara kuiondoa CCM madarakani.
Jussa alitoa kauli hiyo juzi katika mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho Wilaya ya Mjini Unguja Visiwani Zanzibar.
Alisema wametafakari hatua zote kwa yale yanayoendelea nchini na wamejipanga kwa ukamilifu na litakalojitokeza itakuwa ndiyo mwisho wa CCM Zanzibar na Bara.
“Tumetafakari hatua zote na tumejipanga kwa lolote litakalojitokezea, chama chenu kiko imara.
“Wajaribu waone athari zake kwao, tumejipanga kwa ukamilifu na litalokuja kutokea itakuwa ndiyo mwisho wa CCM Zanzibar na Bara.
“Leo hii (juzi) wanaivuruga Chadema, CUF, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi…wanaweza wao wenyewe wakatupeleka tukawa na taasisi moja imara ya kuiangusha CCM Zanzibar na Bara.
“Kwani kuna mtu alifikiria Lowassa (Edward-Waziri Mkuu wa zamani), Sumaye (Frederick-Waziri Mkuu mstaafu) wangehama CCM au kwa hapa Zanzibar kuna siku Mansour (Yusuf Himid-aliyekuwa Mwakilishi wa CCM Jimbo la Kiembe Samaki) angejiunga na CUF?
“Sasa nawaambia wao wanatutazama sisi tu wao wenyewe hawajijui huko ndani, kuna watu wanasema tuko tayari kuungana na upinzani lakini upinzani wenyewe leo umegawanyika.
“… hawa wanaweza wao CCM wakatupa sababu tukaweka jukwaa likavuna wote na likaporomosha CCM kutoka juu mpaka chini, watu wamechoka usifikiri ni sisi tu,” alisema Jussa huku akishangiliwa wanachama hao waliohudhuria mkutano huo.