30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein akemea ubaguzi

Na AMINA OMARI-TANGA


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametaka Watanzania kupiga vita ubaguzi wa aina yoyote miongoni mwao huku wakidumisha umoja na mshikamano miongoni mwao.

Pia amewataka Watanzania wawapuuze watu wanaobeza Muungano kwa lengo la kubaguana kwa kuwa wanaweza kusababisha mpasuko miongoni mwa Watanzania.

Dk. Shein aliyasema hayo  mjini Tanga jana wakati wa kilele cha sherehe za Mwenge wa Uhuru  kwa mwaka 2018 zilizofanyika pamoja na maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere.

Alisema Watanzania hawana budi kuzingatia sifa za msingi za kudumisha umoja na mshikamano zitakazofanya jamii iendelee kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo.

“Hayati Baba wa Taifa, katika falsafa zake alikuwa anasema watu ndiyo msingi wa maendeleo badala ya kutegemea matumizi ya fedha kuwa msingi wa maendeleo.

“Msingi wa maendeleo ni watu wanaojituma kwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu katika kuleta maendeleo ya taifa lao na hayo ndiyo yalikuwa maono yake Hayati Baba wa Taifa,”alisema Rais Dk. Shein.

Aliwataka wananchi kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wahakikishe wanajituma na kuwa wabunifu kuweza kuleta maendeleo ya haraka.

“Serikali itahakikisha inasimamia rasilimali zake zote kwa karibu ziweze kutumika kwa ajili ya kuwanufaisha Watanzania wote kwa ujumla na kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunamuenzi Baba wa Taifa.

“Kama viongozi na wananchi wataweza kuzingaitia wosia wa Baba wa Taifa wa kupinga rushwa kwa vitendo na kujiendeleza katika uchumi nchi hii itaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo.

“Wakati wa uhuru, rais alipania kujenga nchi yenye amani ikiwamo kuheshimu misingi ya utu na kuhamasisha upendo miongoni mwetu.

“Kwa hiyo, kama tutaizingatia misingi hiyo, tutaweza kuleta mshikamano miongoni mwetu,” alisema.

Akizunguzia elimu, Rais Dk. Shein alisema Serikali itaendelea kuweka mkazo kwenye sekta ya elimu kwa kuendelea kufanya maboresho mbalimbali kuleta mabadiliko ya haraka.

“Tumejizatiti kutoa elimu bora bila ubaguzi kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu kwa sababu  kwa kufanya hivyo kutasaidia vijana wetu kupata fursa ya elimu na kuweza kujiajiri.

“Kupitia elimu ndipo nchi itaweza kuzalisha wataalamu mahiri watakaoweza kutafuta ufumbuzi wa majanga kama Ukimwi, rushwa na vitendo vyote vibaya,” alisema.

Wakati huo huo, aliwaasa vijana kupenda kufanya kazi na wasione aibu kwa kuchagua kazi za maendeleo zinazojitokeza kwa sababu taifa linawategemea wao kwa ajili ya kuiendesha nchi.

Kuhusu mwenge wa uhuru, Rais Dk. Shein alisema mbio za mwenge huo zinaendelea kuenziwa kila mwaka hata baada ya utawala wao kwisha.

Alisema katika miaka mitatu ya uongozi wa awamu ya tano, mwenge wa uhuru umezungukia miradi ya maendeleo 4,291 yenye thamani ya Sh trilioni 2.01.

WAZIRI MKUU MAJALIWA

Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,  alitoa siku 10 kwa halmashauri 14 ambazo miradi yao ilishindwa kuzinduliwa na mbio za mwenge kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo rushwa na kuwa chini ya kiwango, kuhakikisha zinawasilisha taarifa za miradi hiyo TAMISEMI.

Alisema taarifa hiyo ianishe  maeneo miradi ilipo na hatua iliyofikia ikiwamo hatua kwa waliohusika na ubadhirifu wa miradi hiyo.

KIONGOZI MBIO ZA MWENGE

Awali, Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Charles Kabeho, akitoa taarifa za mbio hizo, alisema katika miradi mingi waliyoitembelea miradi ya sekta ya maji ndiyo ilionekana ina changamoto nyingi.

Alisema sekta hiyo haijaweza kumkomboa mwananchi wa hali ya chini hususan vijijini kutokana na ukosefu wa maji na miradi mingi haina mafanikio.

Kabeho alisema  kwa miradi ya mwaka huu, waligundua kasoro katika baadhi ya miradi ambayo ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma na baadhi ya miradi kutokwenda  sawasawa na fedha zilizotolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles