Na JUDITH NYANGE-MWANZA
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema mpaka sasa bado ana imani ataapishwa kuwa Rais wa Zanzibar.
Kwamba Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein hatofika mwaka 2020 akiwa kiongoza Serikali.
Ameyasema hayo jijini Mwanza jana, alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Tujadiliane kinachoratibiwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC) na kurushwa na vituo mbalimbali vya redio jijini hapa.
Alisema mpaka sasa, kwa hali ilivyo ana matumaini makubwa ya kuapishwa kwa sababu yeye ni mtu asiyekata tamaa.
Maalim Seif alisema alipozungumza na waandishi wa habari Agosti, 2016 alikuwa na matumaini ataapishwa kuwa Rais wa Zanzibar baada ya miezi mitatu.
Alisema aliamini mchakato uliokuwa unaendelea ulionyesha kila dalili ya kupewa Serikali na kwamba hadi sasa bado ana matumaini hayo.
“Ubabe unaofanywa na CCM Zanzibar una mwisho wake na huo mwisho hauko mbali, kama Afrika Kusini watu walidhani Serikali ya Ubaguzi haitaondoka lakini iliondoka na waliweza kuiondoa na kuweka Serikali yao, hata Zanzibar hilo litawezekana,” alisema.
Maalim Seif alisema ikifika mwaka 2020 bila mabadiliko Zanzibar, anaamini hakutakuwa na uchaguzi mkuu katika visiwa hivyo.
Alisema ameisikia mpango wa CCM ambao ni kusubiri hadi 2019 ndiyo watake mazungumzo, jambo yeye hatalikuba kwa sababu yeye na wenzake si watoto wadogo wa kuhadaiwa.
Akizungumzia taarifa za kuhusu kuwepo vikao baina yake na Rais Dk. Shein, chini ya jumuiya za kimataifa kutafuta suluhu ya hali ya kisiasa Zanzibar, alisema ni minong’ono na uzushi usiokuwa na ukweli wowote na kukumbusha kuwa alipata kukataa kupeana mkono na Rais Shein hivyo haoni sababu ya kuzungumza naye.
Alisema amekuwa akitafuta nafasi ya kuzungumza na Rais Dk. John Magufuli na wiki iliyopita, alimwandikia barua ambayo hata hivyo haijajibiwa lakini bado ana dhamira ya dhati ya kukutana naye.
Alisema kama Rais Magufuli hataki kutatua mgogoro uliopo Zanzibar, hakuna ufumbuzi utakaopatikana kwa yeye kukaa na Rais Dk. Shein.
“Rais Magufuli kama yupo ‘serious’ na anayosema kwamba yeye ni muadilifu, amalize mgogoro wa Zanzibar, mimi nipo tayari kabisa kukutana naye kuzungumzia suala hili lakini kama hataki, hakuna ufumbuzi wa suala hili kwa sababu hakuna mwingine wa kulizungumzia, Dk. Shein anaendeshwa tu hana maamuzi katika suala hili,” alisema.
Akizungumzia kukosa uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar, alisema nje ya Serikali wamefanya vizuri na wananchi wanaona Serikali ya Rais Shein si lolote si chochote na hasa kupitia ziara yake aliyoifanya katika Visiwa vya Unguja na Pemba.