UKUAJI wa mwili na akili kwa pamoja unahitaji ulaji wa mlo kamili ambao utajumuisha aina zote za vyakula ambavyo vinahitajika katika mwili.
Mlo kamili ni ule ambao unajumisha makundi matano ya vyakula. Makundi hayo ni kama vile nafaka, mizizi na ndizi, kundi la pili (vyakula vyenye jamii ya kunde na vyenye asili ya wanyama), kundi la tatu (mbogamboga), kundi la nne (matunda) na kundi la tano (mafuta na sukari).
Aina zote hizi za vyakula ni muhimu katika kujenga afya ya mwili na akili kwa binadamu wa rika zote. Aidha, uhitaji kwa maana ya kiwango kinachoweza kuhitajika mwilini kinaweza kutofautiana kwa kutegemeana na mambo mbalimbali kama vile mtu anapokuwa mgonjwa, uhitaji katika mwili wake unaongezeka ili kuweza kurekebisha mifumo ya mwili pamoja na kusaidia katika kupambana na magonjwa.
Pia kwa kundi la watoto wadogo ambao bado ukuaji wao upo katika kutegemea lishe bora ili waweze kukua vizuri, ulaji wa mlo kamili ni muhimu sana.
Kwa kundi la mama mjamzito, siku zote uhitaji wa mwili ni mkubwa. Mwili wa mama mjamzito unahitaji nyongeza au kuwa na ziada ya vitu mbalimbali ili kumwezesha kuwa katika afya imara pamoja na kuimarisha afya ya mtoto. Lakini kikubwa pia ni ili kumwezesha kupata uzazi salama muda wa kujifungua utakapofika na hata baada ya kujifungua aweze kuendelea kuwa na afya imara.
Miongoni mwa mapungufu ambayo huwa yanajitokeza katika afya ya uzazi ni pale ambapo maandalizi ya kutosha yanakosekana kwa mama hususani kabla ya kupata ujauzito.
Hii yawezekana ikachangiwa na kukosekana kwa elimu ya kutosha katika jamii kuhusu afya ya uzazi na ushirikishwaji wa pande zote mbili katika kujiandaa na matokeo ya ujauzito. Pande mbili kwa maana ya baba na mama.
Wajawazito wengi wamejikuta wanapata matatizo ya meno bila ya kufahamu pengine tatizo hilo linaweza kuwa limesababishwa na nini. Tukumbuke ya kuwa, meno ni mifupa.
Ili mwili uweze kuwa na mifupa imara, unahitaji kupata madini na virutubisho vingine ili iweze kujengeka imara kwa kiwango kinachohitajika.
Kwa mama mjamzito kutokana na kuongezeka uhitaji wa mwili katika madini na virutubisho vingine, endapo kutatokea na upungufu wa aina yoyote ile, basi kutaathiri mifumo ya mwili wa mama pamoja na ukuaji wa mtoto.
Mama mjamzito ili aweze kuendelea kuwa na mifupa imara ikiwa ni pamoja na meno, anahitaji kiasi cha kutosha cha madini ya calcium ili kuimarisha mifupa yake. Aidha, katika kuhakikisha kuwa madini haya yanachukuliwa vizuri tumboni kutoka katika vyakula ambavyo vinatumika kila siku, matumizi ya vyakula vyenye virutubisho vya Vitamini D ni muhimu. Vitamini D husaidia katika kukusanya na kusambaza madini ya Calcium katika mifupa mwilini na kuiimarisha. Vitamini D hupatikana katika vyakula kama vile mayai, samaki, uyoga, maziwa na mafuta ya samaki.
Madini ya Calcium hupatikana katika vyakula kama vile samaki (mifupa ya samaki), dagaa, maziwa/mtindi, ufuta na maharagwe.
Utumiaji wa vyakula hivi kwa pamoja husaidia katika kuimarisha afya ya mifupa pamoja na meno. Kutokana na wajawazito wengi miili yao kukosa madini haya kwa kiwango cha kutosheleza, husababisha wapatwe na matatizo katika mifupa yao ikiwemo meno. Upungufu utasababisha mama mjamzito kuwa na meno ambayo si imara na hatimaye huweza kupoteza jino au meno.
Aidha, ulaji mzuri pia utasaidia katika kuimarisha uwiano wa homoni mwilini ambazo pia husaidia katika kutawala ukuaji wa mwili sambamba na namna ambavyo mifumo ya mwili inafanya kazi.