NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
DAKTARI Mfawidhi wa Gereza la Keko, Dar es Salaam, ameeleza jinsi mfanyabiashara, Yusuf Manji, alivyokuwa akiteseka kwa maumivu alipokuwa gerezani humo, huku kwa siku akimeza vidonge 25 hadi 30.
Alitoa maelezo hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jana wakati hukumu ya mfanyabiashara huyo inatarajiwa kutolewa Oktoba 6 mwaka huu.
Akitoa ushahidi wake katika kesi ya matumizi ya dawa za kulevya inayomkabili Manji, Daktari Mfawidhi wa Gereza la Keko, Inspekta Eliud Mwakawanga (49), alidai afya ya mfanyabiashara huyo akiwa gerezani haikuwa nzuri na kuna kipindi alikuwa anaamka akiwa amechanganyikiwa.
Dk. Eliud alitoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, akiwa shahidi wa sita wa upande wa utetezi.
Akiongozwa na Wakili wa Manji, Hajra Mungula, alidai alimpokea Manji Julai 6 akitokea Hospitali ya Taifa Muhimbili na alipokelewa kama mshtakiwa huku akiwa mgonjwa.
“Tulikaa naye gerezani tangu tulipompokea hadi alipoachiwa, hali ya afya yake akiwa gerezani haikuwa nzuri sana, alikuwa anatumia dawa wakati wote.
“Alikuwa anatumia dawa za crestor, abberall, percoceg, bicodin, xanax na diazepam ambazo alitoka nazo Muhimbili na nyingine tulimpa gerezani kutokana na alichokuwa anachoumwa siku hiyo.
“Manji alikuwa akimeza vidonge kuanzia 25 mpaka 30 kwa siku, kuna kipindi anaamka anatetemeka, amechanganyikiwa… kuna muda anashindwa kutembea kwa maumivu ya mgongo.
“Manji alikuwa anafunga mkanda kwa ajili ya kunyoosha mgongo na alikuwa anakosa hamu ya kula. Kwa maadili, ugonjwa ni siri ya mgonjwa lakini Manji ni mtu anayeumwa mara kwa mara, “alidai Dk. Eliud.
Alidai Magereza walikuwa wakitunza dawa hizo na walikuwa wakimpa zilipokuwa zinahitajika na dawa ikikosekana gerezani alikuwa akiandikiwa cheti kwa ajili ya kununua dawa nje ya magereza.
Shahidi wa saba wa upande wa utetezi kutoka Hospitali ya Temeke ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya akili na dawa za kulevya, Dk. Francis Benedict, alidai kwamba kuna aina ya dawa ambazo mgonjwa anaweza kutumia lakini matokeo yake yakaonyesha anatumia dawa za kulevya.
Alidai mgonjwa akitumia baadhi ya dawa ambazo Manji anatumia, akipimwa mkojo, unasoma anatumia dawa za kulevya kwa sababu itasoma mophine ama benzodiazephine.
Shahidi wa tano ambaye ni Katibu Muhtasi wa Kampuni ya Quality Group Limited, Maria Rugarabamwa, alidai anamfahamu Manji kwa miaka 19.
Alidai anamfahamu kwamba ni mchapakazi, anafanya kazi muda mrefu na kwamba alikuwa akitumia sigara ambazo yeye ndiye huzitunza na humpa anapohitaji kuvuta.
Shahidi huyo alidai ‘aliprinti’ ripoti ya daktari kutoka Marekani ambayo ilikuwa ikielezea dawa anazotumia Manji na alipeleka ripoti hiyo kwa polisi.
Maria aliomba kutoa ripoti hiyo kama kielelezo mahakamani lakini Wakili wa Serikali Mkuu, Timony Vitalis alipinga akidai haiwezi kuaminika kama kweli ilitoka kwa daktari Marekani.
Mahakama ilikataa kupokea ripoti hiyo badala yake ikapokelewa kwa utambuzi.
YALIYOJIRI JUZI
Juzi, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na tiba kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, Dk. Mustapha Bapumia, aliieleza mahakama hiyo kuwa Manji ana vyuma vinne katika moyo wake.
“Nashangaa kuona Manji ana umri mdogo ana vyuma, anatembea kwenye kamba nyembamba na yuko hatarini, ajiangalie,” alidai.
Dk. Bapumia akiongozwa na Wakili wa Manji, Hajra Mungula kutoa ushahidi, alidai alikutana na Manji Februari 21, mwaka huu baada ya kupelekwa hospitalini hapo akiwa na maumivu ya moyo.
Alidai alimpokea Manji na tatizo la moyo ambalo ni tatizo sugu na alizibuliwa mishipa inayopitisha damu kwenye moyo India, Dubai na Marekani na mishipa mitatu tayari ilikuwa imerekebishwa.
“Tulimshauri Manji na timu yangu azibuliwe mishipa lakini alikataa na kusema kuwa tuiache kwa sababu familia yake ipo Marekani na matibabu yake hufanyika huko, hivyo akaomba apatiwe dawa,” alidai shahidi.
Dk. Bapumia alidai walimwandikia Manji atumie dawa nne ambazo ni za kupunguza mafuta, hofu na usingizi na maumivu sugu ya mgongo.
Alidai Manji aliruhusiwa Machi 14, mwaka huu, na siku hiyo hiyo usiku alirudishwa tena hospitalini hapo na aliridhia kurekebishwa vyuma vilivyopo kwenye moyo.
“Kwa wagonjwa wenye matatizo ya moyo, saratani na wenye maumivu makali na wanakosa usingizi, hupewa dawa zenye morphine kwa ajili ya kupunguza maumivu makali na dawa hizi ikitokea mgonjwa akapimwa, inaonyesha kuwa alitumia dawa za kulevya,” alisema Dk. Bapumia.