32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

DEFOE: NENDA BRADLEY LOWERY, SIRI YAKO ITABAKI MOYONI MWANGU

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO



“NENDA Bradley Lowery, mpambanaji, utaendelea kuwa katika moyo wangu hadi mwisho wa maisha yangu, ulinifanya niwe karibu na familia yako kwa kiasi kikubwa, lakini leo hii hayupo tena nami? kapumzike pema peponi,” ndivyo alivyoanza kusema Jermain Defoe baada ya kutangazwa kwa kifo cha Bradley Lowery.

Bradley Lowery alikuwa mtoto mwenye umri wa miaka sita, shabiki wa kutupwa wa klabu ya Sunderland ambayo imeshuka daraja Ligi Kuu nchini England mwishoni mwa msimu uliomalizika hivi karibuni.

Aliteseka sana na ugonjwa wa Saratani ya damu ambayo ilikuwa inashambulia sehemu kubwa ya mifupa yake, mateso aliyoyapata yaliwafanya mashabiki wa soka wa Sunderland pamoja na wadau wa soka duniani kote kuguswa na hali yake.

Alianza kugundulika kuwa anaugua ugonjwa ambao kitaalamu unajulikana kwa jina la ‘NEUROBLASTOMA’ tangu akiwa na miezi 18 baada ya kuzaliwa kwake, hivyo kipindi chote hadi mwishoni mwa wiki iliopita anapoteza maisha bado alikuwa anaugua.

Ameteseka sana katika maisha yake, lakini hakushindwa kuonesha mapenzi yake ya kuishabikia klabu hiyo ya Sunderland, hasa alikuwa anaguswa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo Jermain Defoe.

Mara kwa mara mtoto huyo hali yake ikiwa mbaya Defoe pekee ndiye aliyekuwa na nafasi ya kwenda kumuona akiwa kitandani na hali yake mbaya, kuna wakati aliweza kulala naye pamoja akiwa hospitalini.

Ilisemekana kuwa kitendo cha Defoe kwenye hospitalini mara kwa mara kumtembelea mtoto huyo kulichangia kumpa furaha japokuwa hali yake ilikuwa aichelewi kubadilika.

Desemba mwaka jana mtoto huyo aligonga vichwa mbalimbali vya habari baada ya madaktari kudai hali aliyonayo mtoto huyo hawezi kuishi zaidi ya miezi miwili, hivyo walitangaza kwamba hadi kufikia mwezi wa pili mwaka huu angepoteza maisha.

Kauli hiyo iliwafanya mashabiki wengi kuanza kumjua na kufuatilia hali ya afya yake. Tarehe ambayo ilitajwa kuwa angepoteza maisha, rafiki yake wa karibu Defoe aliombwa kwenda hospitalini kulala pamoja na mtoto huyo ili kumuaga na kushuhudia kifo chake.

Kitu cha ajabu ni kwamba Defoe alipitiwa na usingizi hivyo mtoto huyo alikuwa wa kwanza kuamka asubuhi na kumwamsha mchezaji huyo huku akimwambia ‘Asubuhi sasa kumekucha amka’

Hakuweza kupoteza maisha kama wataalamu walivyodai, lakini hali yake haikuwa sawa mara kwa mara, ila wazazi wake waliamini kuwa hana muda mrefu wa kuendelea kuishi duniani kutokana na hali yake kubadilika huku akilalamika kwamba anapata maumivu makali sana kwenye mifupa.

Wiki mbili zilizopita kupitia kwenye akaunti ya Facebook, mama wa mtoto huyo Gemma, aliandika kwamba hali ya mtoto wake imezidi kuwa mbaya, kasi ya mapigo ya moyo imeongezeka, maumivu ya mifupa, baridi kali na alikuwa anakosa hewa ya kutosha ya Oxygen, hivyo siku zake zitakuwa zimekaribia za kuondoka duniani.

Wiki iliopita familia ya mtoto huyo iliamua kumfanyia sherehe ya kumuaga huku wakiamini kwamba muda wowote anaweza kupoteza maisha, hivyo rafiki mbalimbali wa mtoto huyo na wadau wa soka walijitokeza kumuona kwa mara ya mwisho wakiwa pamoja na Defoe.

“Tunashukuru marafiki wa mtoto wetu kwa kujitokeza kwa wingi, tunaamini Bradley ana furaha ya kuwaona huku akiendelea kupigania uhai wake, lakini tunadhani kuwa sasa ni muda wake wa kuungana na Malaika wa angani, hivyo tunasubiri kuziona pumzi zake za mwisho akituaga,” aliandika mama wa mtoto huyo

Ni kweli, wale waliojitokeza kwenye sherehe hiyo walikuwa watu wa mwisho kumuona kwa kuwa huku sherehe ikiendelea hali yake ilibadilika na kurudishwa hospitalini hadi Ijumaa alipopoteza maisha.

Defoe amedai kwamba siri ya kifo cha mtoto huyo itabaki kuwa moyoni mwake hadi mwisho wa maisha yake, kwa kuwa alikuwa mtu wa karibu na Bradley na familia yake, hivyo kila siku alikuwa anawasiliana na familia juu ya hali ya mtoto wao.

“Nitaendelea kulia kila wakati nikimkumbuka Bradley, ninashindwa kuzuia hisia zangu kwa kuwa nimekuwa nikakaa naye na kujua tatizo linalomsumbua kwa kipindi kirefu, ilikuwa haiwezi kupita siku moja bila ya kuwapigia simu wazazi wake au kumfikilia Bradley.

“Alikuwa na upendo wa kweli kwangu, nilikuwa nauona upendo wake kwenye macho yake kila akiniangalia, nitaendelea kumkumbuka maishani mwangu.

“Picha zake nyingi zipo kwangu, hata nyumbani kwao kuna picha zetu nyingi ambazo tulikuwa pamoja, leo hii ameondoka, ninaamini ipo siku tutaonana,” alisema Defoe

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles