26 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

TAASISI IMARA ZAHITAJIKA KUJENGA UCHUMI WA VIWANDA

Na MWANDISHI WETU


NCHI nyingi zinatamani kuwa na maendeleo katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na afya, elimu, viwanda, ustawi wa jamii na maeneo mengine. Hata hivyo, zipo sababu nyingi zinazokwamisha nchi hasa zinazoendelea kufikia malengo yake ya maendeleo.

Tanzania tangu ilipopata uhuru, Rais wake wa kwanza Julius Nyerere, alitangaza adui watatu wa taifa ambao ni umasikini, ujinga na maradhi. Lakini mpaka sasa adui hao bado wanaendelea kuwepo.

 Alipoingia madarakani mwaka mmoja na nusu uliopita, Rais Dk. John Magufuli aliahidi kubadilisha mwelekeo wa nchi ili kuwezesha watu wake kupata maendeleo na kuinua hali ya maisha ya Watanzania.

Ili kufanikisha azma yake, Rais Magufuli ameamua kuweka msisitizo katika uchumi ya viwanda, njia ambayo anasema itasaidia kuipaisha Tanzania na kuinua maisha Watanzania kwa ujumla.

Pamoja na mambo mengine, Serikali imeweka mikakati ya kuongeza thamani ya viwanda vya kilimo, usindikaji na uzalishaji ikiwemo viwanda vya nyuzi na nguo katika jitihada za kupambana na umasikini na ukosefu wa ajira kwa vijana.

 Kama njia ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano, wiki iliyopita Taasisi ya Utafiti na Kuondoa Umasikini (REPOA) ilifanya mkutano wao wa utafiti wa mwaka jijini Dar es Salaam. Watafiti, wanasiasa, wanasayansi, wataalamu na viongozi walikutana na kujadili jinsi ya kuboresha na kuimarisha taasisi, ambazo wanasema ndio nguzo katika kufikia ndoto za uchumi wa viwanda.

 Wadau wengi katika mkutano huo walijadili kwa kina namna gani wanaweza au Tanzania inaweza kufikia uchumi wa viwanda kwa kujenga taasisi (kwa maana ya sheria, kanuni na taratibu) zitakazoweza kusimamia na kusukuma mbele uchumi wa viwanda.

Msemaji mkuu alikuwa Profesa nguli wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani, Lant Pritchett ambaye alisema kwamba udhaifu wa taasisi umefanya mataifa mengi ya bara la Afrika kushindwa kufanikisha ndoto zao za maendeleo ya viwanda.

 “Nchi nyingi zinazoendelea zinaishi bila taratibu za kisheria, zinaendeleza mambo yake bila kanuni, ndo maana viwanda vimekufa na zinashindwa kupiga hatua.

 “Nchi hizi zinaishi kwa kutumia njia za ‘Dili’ na si sheria na kanuni. Katika mifumo ya dili, kinachoangaliwa si mpango wa uwekezaji, bali wewe ni nani unayetaka kuwekeza na umefanya nini kwenye dili hili au lile…” alisema Profesa Pritchet

Mara kadhaa Rais Dk. Magufuli amesikika akisema kuhusu wapiga dili ambao kwa kiwango kikubwa wananufaika na miradi mikubwa ya nchi, bila kufuata sheria, taratibu na kanuni za sekta husika.

 Ili kufanikisha uchumi wa viwanda, Profesa Lant amesisitiza umuhimu kwa nchi zinazoendelea kuimarisha taasisi zake, kuweka kanuni, sheria na taratibu zikazosaidia kulinda masilahi ya umma kwa manufaa ya watu wote.

 Alisisitiza kwamba jitihada za kubadili taratibu za uwekezaji katika sekta ya viwanda na uboreshaji wa taasisi, ni ngumu kuzaa matunda kama nchi zinazoendelea kwa mtindo wa ‘dili’.

 “Ni muhimu kwa Serikali kutambua matatizo yaliyopo kwenye taasisi zake zote na kuanza kutazama wapi wanapofanya vizuri (performance indicators) ili kuweza kufikia uchumi wa viwanda haraka,” alisema Profesa Lant.

 Alisema kwamba nchini nyingi za Kiafrika zinategemea mazingira katika ukuaji wa uchumi na hazina mikakati wala malengo…”ndio maana mikakati mingi inawekwa tu kiholela na baadaye kuondoka kama upepo, kwa sababu hakuna malengo madhubuti wala dira ya muda mfupi au mrefu,” alisisitiza.

Mwakilisha wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Afrika Mashariki, Roeland Van De Geer, alisisitiza umuhimu wa taasisi imara kuanzia kwenye elimu, afya na miundombinu katika kujenga uchumi wa viwanda nchini, kuboresha maisha na kupunguza umasikini.

 “Nchini hizi zinazoendelea zinahitaji taasisi imara zinazoweza kusimamia sheria, taratibu na kanuni ili kuhakikisha uwekezaji au biashara zinafanyika kwa kufuata taratibu za nchi,” alisema.

 Akifungua mkutano huo, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Philip Mpango, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kwa kiasi kikubwa kupambana na rushwa, ufisadi, ubadhirifu wa mali za umma na kurudisha nidhamu ya kazi kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha taasisi zitakazosaidia kusimamia uchumi wa viwanda.

 “Rais Dk. Magufuli ana nia ya dhati ya kujenga uchumi wa viwanda na kujenga taasisi imara zinazozingatia sheria na taratibu za nchi kwa masilahi ya Taifa,” alisema.

 Dk. Mpango alifafanua kwamba ni muhimu kwa mkutano ule kujadili ni kwa namna ngani wanaweza kuunganisha vyombo vya ulinzi na usalama katika kufikia uchumi wa viwanda kwa kuanzia na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

 Kwa upande, Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dk. Donald Mmari, alisema mkutano huo wa siku mbili  umewaleta pamoja wadau na watafiti kujadili jinsi ya kufikia uchumi wa viwanda na maendeleo.

 “Mada kuu ni umuhimu wa kuwa na taasisi imara ili kuweza kusimamia sheria, kanuni na taratibu katika kila sekta na kuchangia ukuaji wa sekta nyingine za usindikaji, kilimo na uvuvi,” alisisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles