Na Waandishi Wetu-DAR ES SALAAM
RAIS Yoweri Museveni wa Uganda ametoa amewataka wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kuwekeza Uganda.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana, alipotembelea viwanda vya Kampuni ya Bakhresa vya unga na juisi vilivyopo Buguruni na Vingunguti.
“Ninapenda kuwakaribisha wafanyabiashara wa Tanzania kuja Uganda kuwekeza kwani kufanya hivyo kutasaidia kuzalisha bidhaa, upatikanaji wa soko pamoja na ajira,” alisema Museveni.
Alitoa kauli hiyo kutokana na mafanikio ya mwekezaji Said Salim Bakhresa aliyewekeza kiwanda cha ngano nchini humo.
Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni za Bakhresa, Hussein Sufiani alisema kampuni hiyo iko mbioni kuongeza utoaji ngano kutoka tani 1,100 hadi kufikia tani 2,000 kwa siku nchini Uganda.
Alisema kutokana na uwekezaji wa kampuni hiyo Uganda, Waganda 650 wamenufaika na ajira mbalimbali ambazo zinasaidia kuwapatia kipato.
Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwaijage alisema Uganda na Tanzania zimeingia makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwamo ya viwanda.
Alisisitiza Watanzania wanaweza kwenda kuwekeza Uganda kwa vile nchi hiyo inalima tani milioni nne za mahindi lakini ina uwezo wa kutumia tani milioni moja pekee, hivyo ni fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kwenda kuwekeza nchini humo.
“Tunawahamasisha wafanyabiashara wa Uganda na Tanzania kuwekeza katika nchi zao kuzalisha, bidhaa na ajira za kutosha kwa wananchi,” alisema Mwijage.
Vilevile, aliwataka Watanzania kushiriki katika uchumi wa viwanda kwa kuzalisha bidhaa zinazotumika viwandani, mfano kwa kulima matunda au mbogamboga.
Rais Yoweri Museveni aliwasili nchini juzi kwa ziara ya serikali ya siku mbili ambako alifanya mazungumzo na Mwenyeji wake Rais Dk. John Magufuli na jana alitembelea viwanda hivyo vya Bakhresa.