24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

MBOWE AFUNGUKA

Maregesi Paul na Evans Magege-Dodoma/Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amefungua kesi ya kikatiba dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, aliyezungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu jana ni kwamba mbali na Makonda pia kesi hiyo itawajumuisha Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda hiyo, Camilius Wambura.

Dk. Mashinji aliendelea kusema kuwa kesi hiyo imesajiliwa kama kesi ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2017 na imefunguliwa katika Mahakama Kuu Masijala ya Katiba (Masijala Kuu).

Katika kesi hiyo, Mbowe anaomba Mahakama Kuu itamke kuwa Makonda hana mamlaka ya kumdhalilisha na kumkamata.

Pia alisema Mbowe ameiomba mahakama itengue kifungu cha 5 na 7 vya Sheria ya Tawala za Mitaa kwa kuwa ni batili na vinakiuka haki za kikatiba.

Dk. Mashinji alisema mbali na kesi hiyo pia wanatarajia kufungua kesi nyingi zenye mwelekeo huo.

“Kweli mwenyekiti kafungua kesi ya kikatiba na zipo kesi nyingi tu zinakuja, kwa sasa wanasheria wamekaa mafichoni kwa ajili ya kufikirishana kisheria zaidi ili kuweza kufungua kesi nyingine za kutosha tu,” alisema Dk. Mashinji.

Awali, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema angemfungulia Makonda kesi mahakamani baada ya kumhusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Pia alisema hatakwenda kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam hadi atakapopewa wito maalumu wa kisheria unaomtaka afike kituoni hapo kwa tuhuma hizo.

Mbowe alitoa msimamo huo mjini hapa jana alipozungumza na waandishi wa habari.

“Nimewaita hapa ili kuzungumzia ule wito wa kijinai uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akinihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

“Katika mkutano huu wa leo (jana), nina mambo matatu ya kuzungumza. Kwanza, ninakanusha kwa nguvu zote kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa sababu katika maisha yangu, sijawahi kujihusisha na biashara hiyo au hata kutumia dawa za kulevya.

“Pili, ni kwamba sisi kama wapinzani, tunakubaliana na mapambano dhidi ya dawa hizo kwa sababu ni hatari katika maisha yetu na tunaona vita hii ilitakiwa ipiganwe miaka mingi iliyopita, lakini kutokana na sababu mbalimbali, haikupiganwa.

“Tatu, ni kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam si polisi na kwa mujibu wa sheria, hana mamlaka ya kuita mtu polisi ingawa yeye ni kiongozi wa mkoa.

“Mimi ni mbunge, mimi ni kiongozi wa chama kikubwa, mimi ni baba, nina mke na watoto, siwezi kukubali mjinga mmoja anichafue bila sababu. Who is Makonda, kama anadhani anaweza ‘kunisamon’ hivi hivi, siwezi kwenda polisi kuhojiwa hadi hapo watakaponiita kwa kufuata utaratibu wa kisheria.

“Kwa hiyo nitamfungulia mashtaka ya ‘defamation’ kama yeye na wala si kama Jamhuri kwa sababu sina tatizo na Jamhuri. Katika hili, nitadai haki yangu katika mahakama za ndani na ikibidi mahakama za nje,” alisema Mbowe.

Kwa mujibu wa Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema Makonda hana fedha za kumlipa kutokana na jinsi alivyomchafulia jina lake.

Kutokana na hali hiyo, alisema atamfungulia mashtaka si kwa sababu ana shida ya fedha bali ni kwa sababu amemchafulia jina.

“Nimejenga ‘reputation’ yangu kwa miaka mingi na nitaendelea kuilinda kwa nguvu zote. Nauliza hivi Makonda anaweza kusafisha jina langu?

“Mimi si mtoto mdogo na hili ndilo tatizo la kuwapa watu vyeo wasiokuwa na busara. Kamwe huwezi kupambana na dawa za kulevya kwa kutaka misifa, nitamshtaki kwa sababu yeye ndiye ana kiherehere.

“Makonda asifikiri watu wanamwogopa kwa sababu ana urafiki na Magufuli, hatumwogopi, hivi atanilipa nini, hana kiwango cha fedha cha kunilipa,” alisema Mbowe kwa kufoka.

Pamoja na hayo, alisema utaratibu wa kutaja watuhumiwa wa biashara za dawa hizo uliotumiwa na Makonda haufai kwa kuwa unawafanya wahusika waanze kuchukua tahadhari.

Katika mazungumzo yake, Mbowe alionyesha wasiwasi wa ripoti iliyotumiwa na Makonda na kusema baadhi ya watuhumiwa aliowataja kama mmiliki wa Yatch Club na Sleep Way si mtu mmoja bali maeneo hayo yanamilikiwa kwa ubia na watu wengi.

Baada ya Mbowe kutoa taarifa hiyo, Sirro, alisema kama hataripoti bila kutoa taarifa ya hudhuru atafuatwa kwa kuwa polisi inataka kumhoji.

 

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema kama Mbowe angekuwa anajihusisha na biashara ya dawa za kulevya, yeye ndiye angekuwa mshirika wake kwa sababu amefahamiana naye tangu akiwa mdogo.

“Kwanza kabisa nampongeza mwenyekiti kwa kutokwenda polisi kuhojiwa kwa sababu kama angeenda kwa kuitikia wito wa Makonda, ningemshangaa kwani Makonda hana mamlaka hiyo.

“Lakini pia, anaposhambuliwa Mbowe, tunashambuliwa wapinzani wote, ndiyo maana ninasema tuko pamoja na yeye katika vita hii.

“Lakini pia, kama Mbowe angekuwa anajihusisha na biashara ya dawa za kulevya, mimi ndiye ningekuwa punda wake kwa sababu aliniibua tangu nikiwa mdogo chuo kikuu.

“Pamoja na hayo, Makonda atuambie ni sheria gani inampa mamlaka ya kuwatangaza watu na kuwataka wakaripoti polisi,” alisema Zitto.

Mwanzoni mwa wiki hii, Makonda aliitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kutaja watu 65 aliodai wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Miongoni mwao yumo Mbowe, Mfanyabiashara Yusuf Manji, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles