26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MKURUGENZI TPA ANUSURIKA KWENDA JELA

Na Kulwa Mzee

-Dar es Salaam

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe, ametiwa hatiani na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh milioni tano ama kwenda jela miaka mitatu kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Mgawe alihukumiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha.

Hata hivyo, Mgawe alinusurika kwenda jela baada ya ndugu na jamaa kutafuta kiasi hicho cha fedha na kulipa faini.

Mshtakiwa mwenzake, Hamad Koshuma, aliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.

Akisoma hukumu hiyo, Mkeha, alisema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi watatu.

Akifafanua kuhusu Mgawe, alisema mshtakiwa alidai kuwa mkataba wa kibiashara aliosaini baina ya TPA na Kampuni ya China Communications Constructions Company Ltd haukuwa na uhusiano na hatua yoyote kwa ujenzi wa gati namba 13 na namba 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mgawe anadaiwa kuingia mkataba huo bila ya kutangaza zabuni kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma, namba 21 ya mwaka 2004.

Hakimu Mkeha alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hakukuwa na tangazo la umma kualika zabuni na kwamba hasara ingeweza kutokea kwa kufanya hivyo lakini wahusika walizuia mapema.

“Mshtakiwa namba moja alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa biashara kwa ajili ya kampuni ya ujenzi kwa kuinufaisha kampuni hiyo,” alisema.

Mkeha alisema mshtakiwa anastahili adhabu kubwa japo haitakiwi kutolewa adhabu nje ya sheria inavyosema.

Pia alisema kwa makosa hayo anatakiwa kwenda jela miaka isiyozidi mitatu ama kulipa faini isiyozidi Sh milioni tano.

Akimzungumzia mshtakiwa wa pili, alisema shtaka na ushahidi wa kosa la kutumia madaraka vibaya linaonyesha kufanyika Desemba 5, 2011 na wakati huo mshtakiwa Koshuma hakuwa Naibu Mkurugenzi TPA na kwamba aliipata nafasi hiyo Juni mosi, 2012 miezi sita baadaye.

Alisema upande wa mashtaka na wapelelezi walitakiwa kujiridhisha katika uchunguzi kwa sababu hilo ni kosa la mpelelezi.

“Mtu hawezi kutumia madaraka vibaya wakati madaraka hayo hakuwa nayo, sikufanikiwa kupata kosa la kutumia madaraka vibaya ili mahakama imtie hatiani mshtakiwa wa pili.

“Nalazimika kumwachia huru mshtakiwa wa pili Koshuma, namtia hatiani mshtakiwa wa kwanza Mgawe kwa kosa aliloshtakiwa nalo,” alisema Mkeha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles