Na HERIETH FAUSTINE,
EMBE ni tunda lenye ladha nzuri na linaweza kuwa ni moja ya sababu ya kujipatia umaarufu katika jamii na kufanya watu wengi kulistawisha.
Kuna aina nyingi za maembe zinazostawisha hapa nchini, miongoni mwa hizo ni pamoja na embe dodo, sindano, boribo na ng’ongo.
Tunda la embe huliwa kama lilivyo lakini pia huweza kutengenezwa juisi ambayo mara nyingi inakuwa na virutubisho vingi.
Pia ni mmea ambao una faida nyingi kuanzia mizizi, shina, majani na pamoja na maua yake.
Majani yatokanayo na muembe hutibu maradhi mbalimbali ikiwamo harufu mbaya ya mdomoni na yanapotumika ipasavyo huwa na uwezo wa kutibu malaria sugu.
Maua ya mwembe huwasaidia akina mama wanyonyeshao ambao hukabiliwa na uhaba wa maziwa.
Pia tunda hilo limesheheni vitamini A, C, D ambao husaidia usanifishaji wa chakula mwilini.
Vile vile kokwa la embe lenyewe husaidia akina mama wenye tatizo la uzazi ambapo unga wake huzibua mirija ya uzazi na kurekebisha mzunguko wa hedhi kwa yule ambaye anakwenda bila mpangilio.
Pia juisi ya embe husaidia kuleta uoni mzuri kwa sababu ya kuwa na vitamin A ambayo huimarisha afya ya macho na kuwasaidia wale wenye macho makavu na wenye uoni hafifu wakati wa usiku.
Juisi inapotumika bila kuwekwa sukari huwa nzuri kwa watu wenye shida ya kisukari kwani huwasaidia kurekebisha sukari ya mwili kuwa sawa pamoja na mapigo ya moyo na kuondoa sumu hatari mwilini.
Pia huimarisha mfumo wa umeng’enyaji wa chakula mwilini na kusaidia kuondoa shida ya ukosefu wa choo hasa pale inapokuwa imechanganywa na embe pamoja na nanasi.