Na Agatha Charles
WATOTO wanne ambao Jeshi la Polisi liliwatia nguvuni kwa tuhuma za kujihusisha na mafunzo ya kigaidi maeneo ya Vikindu, Mkuranga mkoani Pwani, bado wanashikiliwa, huku upelelezi wa kina ukiendelea chini chini.
Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata kutoka katika vyanzo vyake ndani ya Jeshi hilo, zinadai kuwa, watoto hao ambao wana ujuzi wa kutumia silaha nzito, wamefungiwa kwa takribani siku kumi sasa katika seli za Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wakichunguzwa zaidi.
Watoto hao wanaodaiwa kuwa na umri kati ya miaka 12 hadi 16, walitangazwa kukamatwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro, Novemba 16, mwaka huu.
Alipotangaza Kamanda Sirro, alisema pia walikamatwa wanawake wanne waliokuwa pamoja nao katika msitu huo wa Vikindu.
Hadi kufikia leo, watoto hao watakuwa wanatimiza siku 10 wakiwa mahabusu tangu Kamanda Sirro alipotangaza kuwakamata Novemba 16, mwaka huu.
MTANZANIA Jumamosi linazo taarifa zinazodai kuwa, ujuzi wa watoto hao wa matumizi ya silaha nzito na kukabiliana na adui ndivyo vilivyowashtua polisi na hivyo kuendesha uchunguzi wa kina.
Jana gazeti hili lilifika katika ofisi za Kamanda Sirro, ili kufahamu kinachoendelea dhidi ya watoto hao, ambaye alisema upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea.
Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, hatima ya watoto hao itafahamika mara baada ya upelelezi kukamilika.
“Watoto hao bado wako mikononi mwa polisi na hatima yao itafahamika baada ya upelelezi kukamilika, hapo ndio tutajua,” alisema Kamanda Sirro.
Itakumbukwa kuwa, watoto hao walikamatwa na kikosi kazi kinachopambana na uhalifu wa kutumia silaha na ujambazi na walikutwa wakiwa wamekusanywa kwenye nyumba ya mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Suleiman, wakiwa wanafundishwa mambo ya dini na harakati za kigaidi.
Mtoto mmoja kati yao alidaiwa kutoroshwa kutoka familia ya Shabani Abdallah Maleck, ambaye ni mkazi wa Kitunda, huku ikidaiwa kuwa watoto hao waliachishwa shule tofauti walizokuwa wanasoma jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo ya Kamanda Sirro, ilisema sanjari na mafunzo ya madrasa, pia wamekuwa wakifundishwa ukakamavu, ikiwemo karate, kung-fu na judo na kufundishwa jinsi ya kutumia silaha aina ya SMG na bastola.
Kamanda Sirro alisema wakati huo kuwa watoto hao walifundishwa namna ya kupiga teke la kummaliza mtu pumzi na kufa kwa haraka wakati wa mapigano kumdhibiti adui, kulenga shabaha kwa kutumia risasi, kutumia kitako cha bunduki na singe.
Taarifa hizi za watoto zimekuja wakati ambako gazeti hili liliwahi kuripoti juu ya kuwapo kwa kikosi maalumu cha wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kinachoshirikiana na makachero wa Idara za Usalama kupambana na watu wanaoaminika kutekeleza vitendo vyenye sura ya kigaidi, wanaosadikiwa kujificha katika misitu ya Kisarawe na Mkuranga, ambacho kimebaini uwepo wa kambi tatu kubwa za kigaidi katika ukanda wa Pwani ya Tanzania.
Kubainika kwa kambi hizo kulikuja baada ya msako na mapambano ya siku kadhaa yaliyowahi kufanywa zaidi ya mwaka mmoja uliopita na wapiganaji wa JWTZ, katika maeneo ya mikoa ya Pwani ya kuwasaka wahalifu ambao walifanikiwa kuwatia nguvuni magaidi watano na kukamata bunduki 16 na Sh milioni 170, zilizokuwa zimefichwa chini ya handaki huko Mkuranga.
MTANZANIA Jumamosi liliwahi kudokezwa kuwa, watu waliokamatwa ni washirika wa mtandao uliojengwa chini ya nguzo za imani moja ya dini (jina lake tunalihifadhi), wenye lengo la kuwakomboa waumini wenzao waliodai wanaonewa, huku wengi wao wakiwa wamesweka gerezani bila hatia.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, watu hao wana ngome kubwa tatu katika mikoa ya Morogoro, Lindi na Pwani, katika maeneo ya Kisarawe na Mkuranga, ambako pia kuna idadi kubwa ya wanachama makundi hayo.