27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

WAKURUGENZI NA MAMENEJA ATCL WAPANGULIWA

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM


 

ladislaus-matindiBODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Ndege nchini (ATCL) imewaondoa katika nyadhifa zao wakurugenzi wote waliopo katika menejimenti na baadhi ya mameneja, baada ya kubainika kuwa na kasoro za kiutendaji na kielimu.

Uamuzi huo, ambao hautamhusisha  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Ladislaus Matindi, ulitolewa katika kikao kilichofanyika Novemba 18, lengo likiwa ni kuboresha muundo wa ATCL, ili kukidhi matakwa ya muda mfupi wakati muundo wa kudumu ukiandaliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya shirika hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Mhandisi Emmanuel Korosso, alisema katika kikao hicho bodi iliamua kuwaengua wakurugenzi watano waliokuwa katika idara mbalimbali, ikiwamo ya biashara, ambayo ilikuwa na kaimu.

Mhandisi Korroso alitaja idara nyingine ambazo wakurugenzi wameondolewa  kuwa ni fedha, usalama, ufundi na uendeshaji, ambayo mkurugenzi wake alikuwa anaelekea kustaafu.

“Kwakuwa wakurugenzi wengi walikuwa wanakaimu  nafasi hizo, tumeamua wakurugenzi wanaokaimu warudishwe katika nafasi zao  za chini, ambazo si menejimenti au wahamishiwe katika vituo vya mikoani,” alisema Mhadishi Korosso.

Alisema bodi pia imeagiza  kuondolewa kabisa katika shirika hilo wakurugenzi na mameneja waliothibitishwa ili waweze kupangiwa majukumu mengine yatakayoendana na sifa walizonazo.

Alisema kikao hicho pia kimemuagiza Mtendaji Mkuu kutangaza mara moja nafasi za wakurugenzi na mameneja zilizo wazi kwa kufuata muundo uliopitishwa.

Mbali na hilo, Mhandisi Korosso alisema kwa sasa shirika hilo limeweza kuongeza nidhamu katika mapato na matumizi, jambo ambalo limechangia kuanza kulipa baadhi ya madeni wakati Serikali ikisubiri uhakiki umalizike ili iweze kuyachukua.

“Tumeweza kudhibiti mapato na matumizi vizuri, kumekuwa na ongezeko la mapato ya uzito wa ziada wa mizigo kutokana na usimamizi mzuri, ukusanyaji wa mapato kutoka vituoni na mawakala umeboreshwa sana kutokana na ufuatiliaji wa karibu wa mauzo,” alisema Mhandisi Korosso.

Aliongeza kuwa, bodi pia imetoa ruhusa kwa wafanyakazi na familia zao kupewa tiketi bure mara moja kwa mwaka kama stahiki ya likizo na tiketi yenye punguzo mara moja kwa mwaka.

Kampuni ya ATCL, ambayo awali ilikuwa haina ndege hata moja, ilianza kufanya  kazi za safari za ndege Oktoba 14, mwaka huu, baada ya Serikali kununua ndege mbili mpya aina ya Bombardier Q400.

 

Mwisho.

 

JKCI wafanya upasuaji mwingine mkubwa wa moyo

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

KWA mara ya kwanza nchini, Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imefanya upasuaji mwingine wa kupandikiza mshipa wa damu kwenye moyo wa mgonjwa, ukiwa haujasimamishwa.

Upasuaji huo umefanywa na madaktari bingwa wa taasisi hiyo, kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Open Heart Surgery’ya nchini Australia.

Akizungumza na waandishi wa habari jana hospitalini hapo, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa JKCI, Dk. Bashir Nyangassa, alisema upasuaji huo unajulikana kitaalamu kama ‘Bypass graft’.

“Mishipa ya moyo ya mgonjwa huyu ilikuwa imeziba kabisa, awali ili tuweze kuzibua tulilazimika kusimamisha moyo wake kwa kutumia mashine ya mapafu na moyo ili kufanikisha upasuaji huo. Lakini awamu hii hatukuitumia kabisa mashine hiyo,” alisema.

Alisema kufanyika kwa upasuaji wa aina hiyo nchini kumesaidia kwa kiasi kikubwa, kwani madaktari walioshiriki wamevuna ujuzi kutoka kwa wenzao wa Australia.

“Tulishirikiana nao tangu Novemba 19 hadi 25, mwaka huu, hii ni kambi ya 10 ya upasuaji hapa JKCI, katika kambi hii tumewafanyia upasuaji jumla ya wagonjwa 17,” alisema.

Daktari huyo alisema kati ya wagonjwa hao, 12 ni watoto, watu wazima wakiwa saba pekee na kwamba kati ya hao 17, watatu walifanyiwa upasuaji bila kufungua kifua.

“Bado kuna mamia ya wagonjwa wanaosubiri upasuaji, hasa watoto, tunatamani kuwahudumia wote, lakini tunashindwa kutokana na ufinyu wa nafasi,” alisema.

Alisema bado kuna mamia ya wagonjwa wanaosubiri kupewa huduma, huku jengo lao likiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 100 pekee.

“Kila mwaka tunaona idadi ya wagonjwa ikizidi kuongezeka, hadi sasa kwa mwaka huu tumefanya upasuaji kwa wagonjwa 345, idadi hii imevunja rekodi ya miaka yote huko nyuma, kwani tulikuwa tukiona wagonjwa 100.

“Watu wameanza kuelimika na kuja hospitalini, tumeweza kuokoa fedha nyingi za Serikali ambazo zingetumika nje kwa matibabu kuokoa maisha yao.

“Hivyo tunaiomba Serikali na wadau waweze kutusaidia angalau kupata jengo maalumu kwa ajili ya watoto lenye uwezo wa kuchukua tena vitanda 100,”alisema.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto wa taasisi hiyo, Godwin Sharau, alisema kila mwaka watoto wapatao milioni 1.5 duniani huzaliwa na tatizo la moyo.

“Kwa kukadiria takwimu hizo, Tanzania watoto 15,000 walizaliwa na tatizo hilo kwa mwaka jana pekee, kwa upande wa watu wazima sababu zipo nyingi, ikiwamo ulaji usiofaa, hasa nyama choma,” alisema.

MWISHO

 

 

Tanesco yahatarisha maisha ya wagonjwa

 

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MASHINE za Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) zipo hatarini kuungua, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kukatika ovyo kwa umeme unaosambazwa hospitalini hapo na Shirika la Umeme nchini (Tanesco).

Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Taasisi hiyo, Dk. Bashir Nyangassa, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari.

Alisema kwa siku umeme unaweza kukatika kati ya mara tatu, tano au zaidi, hali ambayo pia humuweka katika hatari ya kupoteza maisha mgonjwa anayekuwa akifanyiwa upasuaji kwa wakati huo.

“Hii ni changamoto kubwa inayotukabili, kweli tunalo jenereta la dharura, lakini hali imekuwa si nzuri, kwani mnaweza kumuingiza mgonjwa kwenye kipimo, ghafla umeme ukakatika, tena si mara moja, kila mara, ni hatari.

“Mashine zetu ni kubwa na za gharama ya juu, kwa mfano ile ya ‘cath lab’, ipo ambayo inatumia betri, tunajiuliza ikitokea zikaungua na au betri zake kufa itakuwaje, tutafanyaje,” alihoji.

Daktari huyo aliliomba Shirika hilo ikiwezekana waweke transfoma itakayotumiwa na taasisi hiyo pekee.

MWISHO

 

 

 

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles