23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI AICHIMBA MKWARA BODI CHUO CHA MAJI

Na JOHANES RESPICHIUS


 

mhandisi-gerson-lwengeWAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, ameitaka Bodi ya Chuo cha Maji kufanya kazi ya kukiboresha chuo hicho kwa kasi na kama haitaweza kufanya kulingana na matarajio yake, anaweza kuivunja muda wowote.

Waziri Lwenge aliyasema hayo jana, jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi mpya ya chuo hicho.

Alisema kwa kuwa wajumbe wa bodi walikubali uteuzi wake, wanatakiwa kuendana na kasi ambayo inahitajika ya kuhakikisha wanaboresha chuo hicho kulingana na wakati uliopo.

“Kwa kawaida huwa tunateua bodi kwa miaka mitatu, lakini kwa utaratibu wangu nataka ‘performance’ zaidi kuliko kuweka muda, kwahiyo kama bodi hamtaweza kwenda na matarajio ninayoyataka naweza kuivunja wakati wowote.

“Kwasababu mmekubali kwenda na kasi ambayo naitaka ya kuhakikisha mnaboresha chuo hiki kwa kutoa wanafunzi walioiva, mmeona Serikali inavyoendelea kuwawekea miundombinu mizuri, kuna mitambo hapa ukienda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakuna, hivyo ninafuatilia na nitaendelea kufuatilia utendaji wa bodi hii kwa ukaribu  sana,” alisema Waziri Lwenge.

Kutokana na azma ya Serikali kutaka kuhamia Dodoma, Mhandisi Lwenge alisema jengo linalojengwa Ubungo, Dar es Salaam la Maji House italitoa kwa chuo hicho kuendesha shughuli zake, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa.

“Suala la majengo tutaliboresha, tunajenga jengo la Maji House tutawakabidhi, sisi tunahamia Dodoma, kwahiyo tumeshawekeza kwa ajili yenu ili kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wengi.

“Kwenye awamu ya kwanza ya programu ya sekta ya maji, hadi kufikia Juni mwaka huu miradi ya maji 1,210 vijijini ilitekelezwa. Kukamilika kwa miradi hii kumetuwezesha kufikia asilimia 72 ya watu kupata maji safi na salama.

“Katika mwaka 2016/2017 jumla ya miradi 386 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Lengo letu ni kufikia asilimia 80 ya watu waishio vijijini ifikapo mwaka 2020,” alisema Mhandisi Lwenge.

Awali akitaja changamoto zinazokikabili Chuo hicho, Mwenyekiti Mteule wa bodi hiyo, Profesa Felix Mtalo, alisema kuna upungufu wa madarasa na mabweni.

“Mwaka 2008 wakati huo kinabadilishwa kuwa Wakala wa Serikali, kikiwa na wanafunzi wasiozidi 200, mwaka huu kina jumla ya wanafunzi 1,922, ambapo mabweni yaliyopo yana uwezo wa kupokea wanafunzi 700 tu, hivyo zaidi ya wanafunzi 1,000 inabidi waishi nje ya Chuo,” alisema Profesa Mtalo.

Alisema changamoto nyingine ni pamoja na ukosefu wa maabara za kutosha, mfano maabara ya ‘Hydrogeology and Water Well Drilling’, kwa ajili ya kozi za uchimbaji visima pamoja na ‘Soil Plant’ (uhandisi wa umwagiliaji).

Kwa mujibu wa Profesa Mtalo, kutokana na changamoto hiyo, chuo kimekuwa kikilazimika kuwapeleka wanafunzi kwa ajili ya uzoefu kwa vitendo kwa Wakala wa Uchimbaji Visima (DDCA) na Taasisi ya Utafiti ya Mlingano, iliyoko Tanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles