UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba, umeliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhama Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam na kurejea Uwanja wa Taifa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo usalama wa afya za wachezaji.
Uamuzi wa Simba unakuja huku wakiwa tayari wameutumia uwanja huo kucheza michezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kufanyiwa maboresho yaliyogharimu Sh bilioni 12 za Tanzania.
Taarifa iliyotumwa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Patrick Kahemele, ilieleza kuwa usalama wa afya za wachezaji wao upo hatarini kutokana na plastiki za kushika nyasi bandia za uwanja huo kukauka, hivyo kuhatarisha afya za wachezaji wanaotumia.
“Kuna haja ya kuufanyia marekebisho uwanja huo kwa kuweka plastiki mpya kutokana na zile zilizopo zilikaa kwa miaka kadhaa bila ya kutumika wakati uwanja ulipokuwa umefungwa kwa maboresho.
“Kwenye mchezo wetu dhidi ya Azam FC uliochezwa hivi karibuni, tumepokea malalamiko pia kutoka kwa mashabiki ambao wamedai walishindwa kuingia uwanjani kutokana na msongamano, hali hiyo inatokana na ongezeko la watu jijini Dar es Salaam na kuongeza mashabiki wanaohitaji kuingia uwanjani,” alisema Kahemele.
Mbali na ombi hilo, Kahemele alitoa wazo la kuwapo kwa mchezo wa kujaribu matumizi ya mfumo wa tiketi za elekroniki, ambalo alipendekeza kufanyika kwa siku tatu, kesho, Alhamisi na Ijumaa.
“Majaribio hayo yatatufanya tutumie vema mfumo huo katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Majimaji kabla ya mchezo wa watani wetu wa jadi timu ya Yanga, kwani bila kujaribu kunaweza kuwa na madhara,” alisema Kamehele.