NA BENJAMIN MASESE, MWANZA
BAADHI ya wananchi wa mitaa ya kata za Lwanima na Kishili wilayani Nyamagana wanachangia maji ya visima vya asili na fisi, ng’ombe na mbweha kutokana na kukosa huduma kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA).
Kitendo hicho kimeonekana kuleta hofu kwa wakazi hao wakidai kupatwa na magonjwa kwa sababu wamekuwa wakikuta vinyesi katika visima vya maji.
Mbali ya magonjwa, wanawake wengi wa mitaa hiyo wamekuwa wakiamka kati ya saa 11.00 na 12.00 ri na kuacha watoto ndani kwa ajili kuwahi kuchota maji na wengine wamekuwa wakikutana na fisi wakiwa visimani, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.
Mpaka sasa tayari familia moja ya Mwarabu Benard imepatwa na athari ya mtoto wao, Profipeli Mwarabu (miezi minane), kufariki dunia hivi karibuni baada ya kuungua moto saa 12.00 asubuhi akiwa ndani ya nyumba wakati mama yake, Honatha Timatheo, akiwa amekwenda kuchota maji katika visima hivyo.
Tukio hilo lilisababisha Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM) na Mkurugenzi wa Mwauwasa, Antony Sanga kwenda katika familia hiyo na kutoa mkono wa pole pamoja na kutembelea mitaa yenye ukosefu wa maji na wakaahidi kupeleka huduma hiyo haraka.
MTANZANIA ilitembelea baadhi ya visima vya asili katika mitaa mbalimbali ya kata hizo pamoja na bonde la linalotenganisha Kata ya Lwanima na Kishili kwa nyakati tofauti na kushuhudia jinsi wanawake wanavyohangaika kugombania maji.
Kisima kimoja cha asili maarufu kinachojulikana kwa jina la Kibundululu ambacho kinatumiwa na wakazi wa Bushitu, Kakebe, Majengomapya na Kilimo, kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi hao lakini ng’ombe wa maeneo hayo wamekuwa wakinywa maji mchana na kujisaidia humo.
Faustina Christopher ambaye ni miongoni mwa wanawake ambao huwahi kuchota maji hayo, alisema analazimika kuwahi alfajiri ili kupata maji masafi.
Alisema wakati mwingine amekuwa akikutana na fisi maeneo hayo.
Edna Samweli, alisema kutokana na kuwa na biashara yake ya mhagawa amekuwa akiwahi kwenda kisimani alfajiri kabla ya ng’ombe kuyachafua kwa vile maji hayo wakati wa mchana yamekuwa yakinuka kinyesi cha mifugo.
Hata hivyo visima vingine vilivyopo bonde linalotenganisha kata za Lwanima na Kishili vimekuwa na idadi kubwa ya wananchi wanaochota maji, huku wafugaji nao wakitegemea kunywesha hapo.
Wakazi hao wameiomba Serikali hususan Mwauwasa, kuwapatia huduma ya maji ikizingatiwa wamekuwa wakiteseka kwa kiasi kikubwa wakati wa kiangazi, kama ilivyo sasa.
Akizungumza na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Mwauwasa, Sanga alisema mamlaka imetenga fedha kwa ajili ya kununua mabomba ya kusambaza maji.
“Tunaomba wananchi watuvumilie kwa kuwa tayari watalaamu wametembelea maeneo hayo na kuchukua takwimu za bomba zinazotakiwa kusambazwa.
“Tutaunganisha maji kutoka Mahina, kupitia Kakebe na kuelekea Majengomapya , Kilimo hadi Kanindo, kazi hii itaanza kufanyika ndani ya mwezi huu,”alisema.