30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi CUF watakiwa kutoa elimu Pemba

Hamad Yusuph Masauni
Hamad Yusuph Masauni

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni, amewataka viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, kusaidia kuelimisha wenzao wa Pemba ambao bado wanaendeleza uhasama licha ya kumalizika   Uchaguzi Mkuu.

Tangu kumalizika   Uchaguzi Mkuu mwaka jana umeibuka ubaguzi baina ya wafuasi wa vyama vya CCM na CUF katika Kisiwa cha Pemba hatua ambayo imesababisha kuzorotesha shughuli za  jamii na  uchumi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Segerea, alisema bado wananchi wa kisiwa hicho wanabaguana katika shughuli mbalimbali ikiwamo misiba.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Diwani wa Segerea (Chadema), Edwin Mwakatobe, Diwani wa Vingunguti (CUF) ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Omar Kumbilamoto na Mbunge wa Segerea, Bonnah Kaluwa (CCM), hatua iliyomshangaza naibu waziri huyo.

“Kule Pemba watu hawazikani lakini hapa nimekuta mseto wa aina yake, Naibu Meya na wenzako saidieni kuelimisha wenzenu, uchaguzi umeisha tuwe kitu kimoja tushirikiane kuijenga nchi yetu,” alisema Masauni.

Alisema hadi sasa kuna upungufu wa vituo vya polisi zaidi ya 4,500 nchi nzima na kwamba hata vilivyopo vingi vimechakaa.

Awali, Mbunge wa Segerea alisema hivi sasa wananchi wanategemea Kituo cha Polisi Stakishari ambacho pia kiko mbali.

“Kwa sasa ili mtu apate huduma ni lazima aende Stakishari ambako ni mbali na kuna msitu mkubwa hapa katikati, hivyo wakati mwingine hata kama unakwenda kutoa taarifa unaweza kuwa muathirika wa uhalifu,” alisema Kaluwa.

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi huo, Joel Kajura, alisema ulianza mwaka 2000 na hadi kukamilika umegharimu Sh milioni 600.

Katika uzinduzi huo pia iliendeshwa harambee ya kuchangia ujenzi huo ambako zaidi ya Sh milioni 7 zilichangwa zikiwa ni fedha taslimu na ahadi. Pia Mbunge Kaluwa alichangia mabati 60 na wadau mbalimbali waliahidi kutoa mifuko ya saruji zaidi ya tani moja kusaidia ujenzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles