27.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 30, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Masauni alitaka Jeshi la Magereza kukubaliana na maboresho ya kimfumo

Na Mwandishi Wetu, MoHA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amesema Jeshi la Magereza lazima likubaliane na maboresho ya kimfumo, kimuundo na kitaasisi ambayo yatakwenda kuongeza uwezo wa uzalishaji mazao ya kilimo kwa magereza ya uzalishaji mali nchini.

Waziri Masauni ameyasema hayo Septemba 29, 2024 alipotembelea na kuzungumza na Maafisa wa Gereza la Kilimo na Mifugo Kitai, Mbinga Mkoani Ruvuma ambapo amesema miongoni mwa maboresho hayo ni kutenganisha mamlaka ya kiutawala ya Jeshi la Magereza na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi hilo (SHIMA), ambapo maboresho yatakwenda kuleta ufanisi wa usimamizi wa mauasala ya kiutawala na biashara.

Katika hatua nyingine Waziri Masauni ametoa maagizo kwa Magereza ya Uzalishaji Mali nchi nzima kuchangamkia fursa za kilimo cha mazao ya nafaka kwa kutanua maeneo ya mashamba ili kuendana na jitihada za Serikali katika kuinua sekta ya kilimo.

“Serikali imetanua fursa ya soko la mazao ya nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ambayo imepewa uwezo na Serikali kununua mazao kwa bei kubwa lakini mpaka sasa bado hakuna jitihada zilizofanywa na Jeshi la Magereza kuchagamkia fursa hii”. Amesema Waziri Masauni.

Aidha amesisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuacha na matumizi ya kuni na mkaa katika magereza ili kuendana na ajenda ya Afrika na Dunia katika kutunza mazingira.

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la Kilimo na Mifugo Kitai, SP. Gabriel Luderi amesema gereza hilo lipo tayari kupokea na kuendana na mabadiliko yakatayoongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Magereza.

Awali Waziri Masauni alitembelea Gereza hilo mwaka 2019 akiwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo ambapo amesema licha ya kuwa sasa kuna mabadiliko lakini alitarajia kuona mabadiliko makubwa zaidi ya Kilimo katika gereza hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles