27.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 28, 2024

Contact us: [email protected]

TPDC yaimarisha huduma za kijamii katika maeneo ya Gesi Asilia

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za kijamii kwenye maeneo ambako shughuli za utafutaji, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia zinafanyika.

Huduma mbalimbali za kijamii kama afya, elimu, maji na utawala bora zinaimarishwa kama sehemu ya Uwajibikaji wa Shirika kwa Jamii (CSR).

Wajumbe wa Bodi ya TPDC, Viongozi wa Halmashauri, Wakandarasi na Timu ya mradi ya TPDC wakiwa katika picha ya pamoja.

Hayo yamebainishwa katika ziara ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC walipotembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na TPDC kupitia mpango wa uwajibikaji wa Shirika kwa Jamii, maarufu kama “Corporate Social Responsibility” mkoani Mtwara.

Akitoa ufafanuzi wa miradi hiyo, Meneja Mradi, Mhandisi Omari Kitiku, amesema, “TPDC ilisaini hati ya makubaliano (MoU) ya utekelezaji wa miradi yenye thamani ya Sh bilioni 1.28 ambayo inatekelezwa katika kata ya Msimbati na Madimba.

Makubaliano hayo yalihusisha Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Msimbati, Jeshi la Polisi Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi cha kata ya Msimbati, pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa ajili ya uwekaji wa taa za barabarani katika vijiji vya Msimbati, Mngoji na Madimba.

Mhandisi Omari Kitiku akitoa ufafanuzi wa maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya kwa wajumbe ya Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC.

Mhandisi Kitiku ameongeza kuwa, “Gharama za ujenzi wa miradi hiyo zinatofautiana kulingana na aina ya mradi. Ujenzi wa kituo cha afya unagharimu Sh 600,000,000 ambapo umefikia asilimia 80 ya ujenzi. Ujenzi wa kituo cha polisi unagharimu Sh 186,170,803 na umefikia asilimia 65, pamoja na uwekaji wa taa za barabarani kwa Sh 498,205,327 ambao umefikia asilimia 15,” amesema Mhandisi Kitiku.

Awali, Afisa Maendeleo ya Jamii wa TPDC, Ally Mluge, alieleza namna TPDC inavyoshirikiana na jamii kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa lengo la kuleta ustawi wa jamii na kuboresha mahusiano mazuri kati ya TPDC na jamii zinazopitiwa na miundombinu ya gesi asilia.

“Utekelezaji wa miradi hii ni sehemu ya jitihada za TPDC katika kukuza na kuboresha huduma na mahusiano na jamii zinazopitiwa na miundombinu ya gesi asilia,” amesema Mluge.

Katika hatua nyingine, Rashidi Omary Linkoni, Diwani wa Kata ya Msimbati, alishukuru uongozi wa TPDC kwa jitihada zao za kuimarisha huduma za kijamii katika maeneo yanayopitiwa na miundombinu ya gesi asilia.

“TPDC, kupitia jitihada zake za kusaidia jamii, inaongeza chachu ya kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma hizo katika maeneo yetu. Kwa hatua hii, naipongeza TPDC na tunaomba iendelee na jitihada hizi,” amesema Linkoni.

Muonekano wa jengo la Kituo cha Polisi cha Msimbati  linaloendelea kujengwa kwa ufadhili wa TPDC.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles