Na Mwandishi wetu.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeendelea kuwaelimisha wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiyari kutumia fidia wanazopata kwa kufanya shughuli za maendeleo ili kuweza kuishi maisha bora na kujitegemea katika maeneo mapya wanayohamia.
Katika mahojiano maalum na mwandishi wetu Kaimu Meneja wa Uhusiano kwa Umma NCAA Bw. Hamis Dambaya amesema pamoja na wananchi hao kupewa shilingi milioni kumi za motisha kwa kila kaya kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan lakini pia hulipwa fidia za maendelezo ambayo ni muhimu wanananchi hao wakaitumia kuendeleza maeneo waliyopewa na serikali.
“Mkuu wa Kaya anaweza kuwa na Boma zaidi ya moja sehemu anapoishi ngorongoro na wakati anaandikisha anapewa fidia ya maboma/nyumba zake zote kwa hiyo anapofika Msomera Serikali inampa nyumba moja kama mkuu wa kaya na familia yake, fedha alizolipwa za fidia ya maboma yake kule Ngorongoro anashauriwa kuzitumia kujenga maboma hayo au nyumba bora zaidi katika eneo la ekari 2.5 analopewa Msomera” amefafanua Dambaya.
Akijibu swali kuhusiana na mawazo ya baadhi ya watu kwamba serikali ina wajibu wa kuijengea kila familia nyumba inazotaka bwana Dambaya amesema jambo hilo halitowezekana hasa kutokana na utaratibu na sheria ya fidia ambacho kinachofanyika wakati wa utoaji wa elimu kwa umma ni kuwaelekeza wananchi wanapolipwa fidia hizo kuona umuhimu wa kuwekeza katika maeneo wanayopewa hasa kilimo, biashara, ufugaji na shughuli zingine za ujasiriamali ili kuwa na maisha bora na kipato endelevu.
Bw. Dambaya ametoa rai kwa kila mwananchi anayetaka kuhama kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kuhakikisha anapata uelewa wa zoezi hilo kabla ya kuhama ili kuepuka migogoro mara baada ya kuhama na kusisitiza kuwa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro itaendelea kusimamia haki ya kila mwananchi katika zoezi hilo.
Taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya wananchi wanaohama kutoka Ngorongoro kwenda Msomera na maeneo mengine wamekuwa wakitumia fedha wanazopata kufanya mambo mengine badala ya kuwekeza katika shughuli za maendeleo jambo linaloweza kusababisha usumbufu kwa familia zao katika maeneo wanayoelekea.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kupitia watalaam wake wa elimu kwa umma pamoja na idara ya maendeleo ya jamii imeendelea kutoa elimu kwa wananchi hao kuhusiana na matumizi bora ya fedha kabla ya zoezi la kuwahamisha kufanyika ili kuwajengea uwezo wananchi wanaohama kwa hiyari kutumia fedha zao kwa usahihi.