33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Zungu: Urais 2025 Samia haondoki

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amesema Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi nzuri zinazoonekana na kuwataka Watanzania kuendelea kumuunga mkono ili aendelee kuiongoza Tanzania katika kipindi kingine.

Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala ameyasema hayo Januari 27,2024 alipokuwa akizungumza na wamachinga wa Mkoa wa Dar es Salaam katika hafla ya kumpongeza Rais Samia katika siku yake ya kuzaliwa.

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, akimlisha keki mmoja wa wamachinga wa Dar es Salaam wakati wa hafla ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan katika siku yake ya kuzaliwa.

“Kocha anayeleta vikombe habadilishwi, mimi timu yangu ni Riverpool kocha wetu ameamua kung’atuka lakini anaondoka na vikombe…mama Samia haondoki kwa sababu anatuletea vikombe vya ushindi na sisi tuko tayari kumuunga mkono.

“Mchango wake kwa taifa ni mkubwa, wote tumuunge mkono mama, tusitetereke na wala tusibabaike,” amesema Zungu.

Meneja wa Machinga Complex, Stella Mgumia, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan iliyoadhimishwa na wamachinga.

Zungu pia amekemea tabia ya baadhi ya askari wa jiji wanaonyanyasa wamachinga na kusema hayo si maelekezo ya rais.

“Mama Samia ametaka utaratibu uwekwe wafanyabiashara wafanye kazi kwa amani, tunapoona mgambo wanaingia mpaka kwa mama lishe kumwaga au kuondoka na vyakula haya si maelekezo ya mheshimiwa rais.

“Kama kuna mtu anataka kumrudisha nyuma rais wetu sisi tutakula naye sahani moja, wanaofanya biashara maeneo ambayo si rasmi jipangeni nendeni kwa mkuu wa wilaya awaelekeze utaratibu wa kisheria,” amesema Zungu.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema jukumu la halmashauri si kupora au kuchukua mali za watu na kwenda kuzihifadhi na kuahidi kuwa wataendelea kupambana na askari wanaonyanyasa wamachinga.

“Hatuwezi kuwa sehemu ya kudhulumu mali za watu, kama mfanyabiashara amekosea aelekezwe mahali pa kwenda kufanyia biashara lakini si wajibu wetu kuchukua mali ya mtu na kwenda kupeleka stoo,” amesema Mpogolo.

Meneja wa Machinga Complex, Stella Mgumia, amesema bado kuna nafasi katika maeneo maalumu yaliyotengwa kufanyia biashara na kuwataka wafanyabiashara kutoka katika maeneo yasiyo rasmi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wamachinga Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Namoto, amesema wanaridhishwa na juhudi zinazofanywa na Serikali kushughulikia kero zao na kuomba waachwe wafanye biashara bila kusumbuliwa.

“Rais Samia alitukaribisha Ikulu akazungumza nasi na kusikiliza changamoto zetu, alitoa fedha za ujenzi wa ofisi za machinga nchi nzima.

“Tunampenda sna tunamthamini ndiyo maana tumetumia siku hii kufanya usafi katika maeneo mbalimbali na kula keki kumpongeza katika siku yake ya kuzaliwa…2024 na 2025 tuna jambo na mama,” amesema Namoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles