Na Ramadhan Hassan, Dodoma
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA) imejipanga kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Bunda ifikapo mwaka 2025.
Hayo yameelezwa Julai 20, 2023 jini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Ester Gilyoma wakati akiwasilisha utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo kwa mwaka 2023/24.
Mkurugenzi huyo amesema upotevu wa maji hasa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ni asilimia 36 ambapo Mamlaka hiyo imeweka mikakati ya kupunguza upotevu huo kwa kuweka mpango wa miaka mitatu katika mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2023/2024 unaoendana na mpango wa kibiashara wa Mamlaka ya maji.
Sambamba na hivyo Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Bunda imeandaa andiko mradi kwa ajili ya kukopa fedha kiasi cha Sh milioni 815 kutoka mfuko wa maji ili kuhakikisha upotevu wa maji unapungua kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024.
Pia, mamlaka hiyo imeomba kuongezewa eneo la utendaji la Mamlaka ya majisafi na usafiwa mazingira Busega,Kibara na Nyamswa nia ikiwa ni kuboresha huduma, kuongeza idadi ya wateja ambao watasaidia kupunguza gharama za uendeshaji na kupunguza gharama ya bili ya maji.
“Kupitia miradi mbalimbali itakayojengwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira itaweza kufikia huduma ya maji kwa asilimia 95 kufikia mwaka 2025,” amesema Mtendaji huyo.
Hata hivyo, amesema Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Bunda haina huduma ya Majitaka, hivyo magari ya watu binafsi ambayo yanasimamiwa na halmashauri ya Mji wa Bunda ndiyo yatatumika katika kutoa huduma.