* Ipo pia tezi dume, homa ya ini
Na Clara Matimo, Mwanza
Wananchi 5000 mkoani hapa wanatarajia kupatiwa huduma ya vipimo bure vya kutambua magonjwa mbalimbali kutoka Chama cha Wanasayansi wa Maabara za Afya (MeLSAT) Mkoa wa Mwanza, ikiwemo viashiria vya saratani ya tezi dume, homa ya ini, kisukari, malaria, shinikizo la damu, kaswende na Virusi vya Ukimwi(VVU).
Hayo yamebainishwa jijini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel April 28, ambapo ameeleza kwamba huduma hizo zitatolewa kuanzia Mei 2 hadi 6, mwaka huu katika uwanja wa furahisha uliopo Manispaa ya Ilemela mkoani humo ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya huduma za maabara kimkoa ambayo yameandaliwa na MeLSAT kwa kushirikiana na ofisi yake huku akiwataka wakazi wa mkoa huo kutumia fursa hiyo adhimu kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali.
Ametaja huduma zingine zitakazotolewa katika maadhimisho hayo kuwa ni elimu kuhusu shughuli za Baraza la Wataalamu wa Maabara (HLPC), maonyesho ya vifaa mbalimbali vya maabara kutoka makampuni tofauti tofauti yanayouza vifaa vya maabara nchini pia wananchi watapata fursa ya kupata ushauri kutoka kwa wataalamu hao.
“Nawasihi wananchi wa mkoa huu watumie fursa hii adhimu wafike uwanja wa furahisha tarehe zilizopangwa ili kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali pamoja na kupatiwa elimu juu ya matumizi sahihi ya huduma za maabara na shughuli zinazofanywa na wanataaluma wa sayansi za afya nchini hasa wanaume wajitokeze kwa wingi wapime viashiria vya saratani ya tezi dume maana utafiti unaonyesha wanaume wengi wanapitia changamoto hizo hasa umri unavyozidi kuwa mkubwa changamoto zinaanza kuonekana wataalamu wa afya wanasema viashairia huwa haviko wazi sana.
“Lakini ukifanikiwa kupima mapema unapata matibabu sahihi na kwa wakati sahihi kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ambapo maisha yako yataboreka, watu wengi tumejikuta tukitembea wakati tuna magonjwa yanatusumbua hadi pale unapofanyiwa uchunguzi wa maabara ndipo itabainika afya yako haiko sawa yapo mashambulizi ya virusi vya magonjwa mbalimbali ya kuambukiza ambayo yanapatikana ndani ya damu hivyo nasisitiza wananchi wengi wajitokeze kwenye zoezi hili muhimu kwa ajili ya kupata matibabu sahihi na bora ili kupunguza gharama zisizo za lazima,” amesema Mhandisi Gabriel.
Amesema uwepo wa maonyesho ya vifaa mbalimbali vya maabara kutoka kwa makampuni tofauti tofauti kwenye maadhimisho hayo yanayouza vifaa hivyo nchini, itakuwa ni fursa kwa baadhi ya maabara za mkoa huo kukutana na wauzaji wa vifaa hivyo kujua teknolojia iliyopo, upatikanaji wake faida na changamoto ya teknolojia zilizopita, hali itakayochangia kuimarishwa kwa maabara zilizopo na utasaidia kuongeza ufanisi wa huduma hizo kwa wakazi wa mkoa wa Mwanza na kanda ya ziwa.
Aidha, Mhandisi Gabriel amewaomba wananchi wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi uwanjani hapo kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu katika hospitali za mkoa huo kwani mahitaji ya damu bado ni makubwa kutokana na idadi ya wahitaji wengi wao wakiwa ni watoto chini ya miaka mitano, akina mama wajawazito, watu wenye magonjwa sugu na wanaopatwa na ajali.
Ametoa wito kw waajiri wote ndani ya mkoa wa Mwanza kuwaruhusu wataalamu wa maabara ili wasshiriki kikamilifu katika tukio hilo muhimu la kitaaluma na bila kuathiri utendaji wa kazi katika maeneo yao.
Mwenyekiti wa MeLSAT Mkoa wa Mwanza, Bertrand Msemwa, amesema lengo la kuandaa maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu afya zao na kuwapa elimu ya majukumu walionayo wataalamu wa maabara ikiwemo kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kwa binadamu na kutoa majibu kwa ajili ya kusaidia matibabu.
“Tumeandaa maadhimisho ili tutoe elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya vipimo kabla ya kumeza dawa ili kuondoa tatizo lililopo dunia nzima la usugu wa dawa linalosababishwa na wananchi kutumia dawa bila kufanya vipimo bora vya kimaabara, makadirio yetu ni kuhudumia wananchi 1,000 kwa siku hivyo nawasisi wakazi wa mkoa huu na mikoa jirani wafike kwenye maadhimisho hayo wapate elimu itakayowasaidia kulinda afya zao,”amesema Msemwa.
Mratibu wa Huduma za Maabara Manispaa ya Ilemela Mkoa wa Mwanza, Isikile Rutashoborwa , amesema wanatekeleza majukumu yao kwa kusimamia miongozo inayowaongoza lengo ni kutoa huduma na vipimo sahihi kwa wanao wahudumia.
Maadhimisho ya wiki ya huduma za maabara hufanyika mwishoni mwa Aprili duniani kote kila mwaka, Tanzania mwaka huu inaadhimisha kwa mara ya 13 ambapo Mkoani Mwanza yatafanyika kwa mara ya kwanza, kauli mbiu inasema ‘vipimo vya maabara za afya ndio msingi wa matibabu bora’, kazi iendelee.