Na Ramadhan Hassan,Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango,Dk.Mwigulu Nchemba amezitaka Halmashauri 55 zilizopokea mikopo ya fedha yenye thamani ya shilingi bilioni 50 kuhakikisha wanazitumia vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa na kuzirudisha kwa wakati ili halmashauri nyingine zipate fursa za kukopa.
Akizungumza leo Novemba 8,2021,jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini ya makubaliano wa utoaji wa fedha za mikopo ya utekelezaji wa programu ya kupanga ,kupima na kumilikisha ardhi nchini,Waziri huyo amezitaka halmashauri hizo kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Waziri Nchemba amesema serikali imetoa kiasi cha sh bilioni 50 kwa halmashauri 55 nchini kupitia wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kusaidia upimaji wa ardhi kwenye maeneo yao.
Amesema lengo la Serikali kutoa mikopo hiyo ni kuziwezesha Halmashauri hizo kupima ardhi ili kuondoa ujenzi holela kwenye maeneo hayo
“Serikali itaendelea kutoa fedha hizo kutokana na hali ya bajeti itakavyokuwa imepangwa hivyo waliopata mikopo hiyo wanatakiwa kuonyesha mifano kwa wengine watakaohitaji,”amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeeo ya Makazi ,William Lukuvi amesema kupitia fedha hizo halmashauri zitaweza kutengeneza bilioni 41 huku akitolea mfano Halmashauri ya Meru imekopa sh bilioni 1.6 na inatarajia kuingiza sh bilioni 7.8.
Waziri Lukuvi amesema siku za nyuma Halmashauri zilikuwa zikiomba mikopo kutoka taasisi za kifedha lakini awamu hii serikali imechuku jukumu hilo.
Amesema mikopo hiyo imetolewa na serikali kutokana na andiko lililoandikwa na Halmashauri husika kuhusu kazi za fedha hizo.
Amesema kuwa jumla ya Halmashauri 78 ziliomba mikopo hiyo lakini waliofanikiwa ni Halmashauri hizo 55 na watakuwa wakitoa mikopo hiyo.
Naye,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Ummy Mwalimu ameagiza mapato ya ndani ya maendeleo katika Halmashauri kutumika pia katika kupima na kupanga miji bila kutaja asilimia ambazo zinatakiwa kutengwa.
Hatua hiyo ilikuja kutokana na Waziri Lukuvi kumuomba Waziri Ummy Mwalimu Halmashuri zitenge fedha kidogo kwa ajili ya kupima na kupanga maeneo.
Waziri Ummy amesema kupatikana kwa fedha hizo kumeongeza vipaumbele alivyokusudia kwenye utendaji wake wa kazi alivyojiwekea wakati anaingi kwenye wizara hiyo.
Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni huduma za afya ,elimu msingi ,kuwawezesha wananchi kiuchumi hasa akinamama ,walemavu na vijana,ujenzi wa miundombinu ya barabara
Waziri Mwalimu amesema kwa sasa ameongezewe kipaumbele cha tano kilichongezewa hiyom jana kuwa ni upimaji ardhi kwenye Halmashauri mbalimbali nchini.
“Upatikanaji wa fedha hizo zitaenda kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi pamoja na Halmashauri husika,”amesema.