23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DK. Gwajima aanika mafaniko Sekta ya Afya nchini miaka 60 ya Uhuru

*Mpango wa Bima ya Afya kwa wote wanukia

*Vituo vya afya sasa kila kona, wataalamu wakiongezeka

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima ametaja mafaniko yaliyopatika katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru upande wa afya huku akidai suala la bima ya afya kwa wote limeishatoka katika mikono yao na kwa sasa lipo Baraza la Mawaziri.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma leo Jumatatu Novemba 8, 2021, wakati akieleza mafanikio ya wizara hiyo kwa miaka 60 ya uhuru, Dk. Gwajima amesema suala la bima ya afya ni muhimu na linahitaji kupita ngazi zote za maamuzi kuanzia wizarani hadi bungeni.

“Suala hili ni kubwa linahitaji kupita ngazi zote za maamuzi, lianze kwenye wizara litoke liende kwa Makatibu Wakuu litoke liende kwenye Baraza la Mawaziri litoke liende kwenye kamati inayoshughulikia mambo ya  kisheria, litoke na kisha liende bungeni.

“Ninachoweza kusema leo suala hili limeishatoka kwenye sekta ya afya lilipokuwa limekwama huko limetoka kwa Speed ya Jet likaenda kwenye ngazi ya baraza la mawaziri hivi ninavyosema tuna kikosi kazi chetu kimeboresha,”amesema Dk. Gwajima.

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima, akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, leoNovemba 8, 2021 kuelezea mafanikio ya miaka 60 ya Uhuru.

Waziri huyo amesema, serikali inaendelea kukamilisha muswada wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote na imefikia hatua kubwa; “Huu ni mwelekeo mzuri wa nchi katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru,”amesema.

KUIMARIKA KWA HUDUMA ZA AFYA

Dk. Gwajima ameyataka mafanikio mengine katika sekta ya afya kuwa ni kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote ambayo imefikia vituo 8,537 ikilinganishwa na vituo 1,343 Mwaka 1960.

Amesema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 84.26 ambapo  kati ya vituo hivyo, serikali inamiliki asilimia 64, Mashirika ya dini asilimia 9 na vituo binafsi asilimia 27.

Aidha, amaebainisha kuwa mtandao wa vituo vya huduma za afya umepanuka na kusogea karibu zaidi na wananchi ambapo zahanati zimefikia 7,242, Vituo vya afya 926 na Hospitali za Wilaya ni 178, na hospitali zingine 151.

Ameendelea kufafanua kuwa, hospitali za kibingwa ngazi ya mikoa ni (28), ngazi ya Kanda sita (6), hospitali za ubingwa maalumu ni tano (5) na hospitali ya taifa ni moja (MNH).

Hospitali ya Uhuru iliyoko jijini Dodoma.

Amesema vituo vyote hivyo vina jumla ya vitanda 90,488 ikiwa ni sawa na ongezeko la vitanda 71,656 sawa na asilimia 79.18.

“Kwa sasa uwiano wa vituo kwa idadi ya watu ni kituo kimoja kwa watu 6,751.5 (1: 6,751.5) tofauti na 1:40,000-50,000 kabla ya uhuru. Hivyo, Tanzania imefikia malengo ya Umoja wa Mataifa katika upatikanaji wa huduma za afya kwa kuzingatia idadi ya watu na Jiografia,”amesema Dk. Gwajima.

“Aidha, uwiano wa vitanda kwa idadi ya watu ni kitanda kimoja kwa watu 637 (1:637) ukilinganisha na 1:1,000 kabla ya uhuru, mwaka 2020 uwiano wa wagonjwa kwa vitanda ulikuwa kitanda kimoja kwa watu 19 (1:19),”amesema Dk. Gwajima.

ONGEZEKO LA WATUMISHI, WATAALAMU

Amesema idadi ya watumishi na wigo wa kada za wataalamu kwenye vituo vya huduma umepanuka kiasi kwamba hivi sasa vituo vya afya vinafanya hadi huduma za upasuaji mkubwa ambao awali ulikuwa haufanyiki.

“Idadi ya wataalamu wa baadhi ya kada mbalimbali za msingi kwenye afya waliosajiliwa imeongezeka hadi kufikia zaidi 71,365 na usajili unaendelea kila siku.

Madaktari bingwa wa moyo wakimfanyia mgonjwa upasuaji

“Hawa ni baadhi tu ya kada zinazojumuisha madaktari bingwa, wa kawaida, wauguzi, wataalamu wa maabara, mionzi, wafamasia na mionzi. Kabla ya uhuru wote hawa kwa ujumla walikuwa 435 tu. Hii ni hatua kubwa sana,”amesema Dk. Gwajima.

KUPANUKA KWA HUDUMA ZA CHANJO

Dk. Gwajima amesema hadi kufikia Juni, 2021 huduma za chanjo zimepanuka na kuimarika na kufanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza kwa ufanisi eneo hili hususan chanjo za watoto chini ya mwaka mmoja (1) huku utekelezaji ukiwa umefikia asilimia 101.

Aidha, kila kituo cha huduma za afya kina huduma ya chanjo kwa ajili ya kinga ya ugonjwa wa Polio (OPV3), PENTA-3 kwa ajili ya kuzuia magonjwa ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda (tetanus), homa ya ini na homa ya uti wa mgongo na chanjo ya Surua/ rubella.

Amesema idadi ya Kliniki za afya ya uzazi imeongezeka na sera ni kuwa katika kila kituo cha huduma za afya kuwe na huduma za afya ya uzazi na mtoto.

“Mifumo ya uongozi na uendeshaji wa vituo vya huduma za afya imeboreshwa kiasi kwamba wananchi nao ni sehemu ya bodi za ushauri katika uendeshaji na kamati za ushauri na uendeshaji kuanzia hospitali za kitaifa hadi zahanati,”amesema.

ONGEZEKO LA VIWANDA VYA DAWA

Amesema hadi kufikia Juni, 2021, Mamlaka ilikuwa imesajili jumla ya viwanda vya ndani 36, ambapo 11 vya dawa, viwanda 14 vya vifaa tiba na 11 vya gesi tiba vinavyofanya kazi ukilinganisha na kiwanda kimoja cha dawa kilichokuwa kimesajiliwa wakati wa Uhuru mwaka 1961.

Ameyataja mafanikio mengine ni  kuongezeka kwa umri wa kuishi wa mtanzania toka miaka 36 mwaka 1961 hadi miaka 66 mwaka 2020 ambayo inaashiria kuimarika kwa mifumo ya utoaji huduma za afya nchini.

“Hili ni ongezeko la mara mbili kwenye umri wa kuishi mtanzania,”amesema.

Taarifa kwa vyombo vya Habari, ni mfululizo wa Wizara kutoa taarifa, mpango unao ratibiwa na Idara ya Habari Maelezo kwa Ushirikiano na Vitengo vya Mawasiliano Serikalini ndani ya Wizara na taasisi, kuelekea miaka 60 ya Uhuru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles