24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Tatueni changamoto ya wafanyabiashara kukimbia soko- DC Kihongosi

Janeth Mushi,Arusha

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi, amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk. John Pima kwa kushirikiana na uongozi wa soko hilo kutatua changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara waliocha meza zao ndani ya soko na kuuza bidhaa zao nje ya soko hilo.
 
Aidha, amewataka wafanyabiashara hao kusimamia na kuzingatia taratibu zilizowekwa.
 
Mkuu huyo ametoa kauli hiyo jana katika Soko Kuu la Arusha, mara baada ya kumalizika kwa kampeni ya usafi wa Jiji la Arusha, lililoongozwa na Mkuu huyo pamoja na kundi la mazoezi la Arusha Jogging Club,na wafanyabiashara hao.
 
Ametoa kauli hiyo kufuatia malalamiko ya wafanyabiashara waliopo katika soko hilo ambao wamedai kuwa baadhi ya wenzao wametoa bidhaa zao nje hali inayowafanya waliopo ndani kushindwa kuuza bidhaa zao.
 
“Nakuagiza Mkurugenzi usimamie utaratibu kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa soko na wale wote wanaohusika kama mtu ana meza yake ndani kwanini aweke meza nje,kama mtu ana kibanda ndani arudi ndani.
 
“Nitasema kwanini tumekuja kufanya usafi leo.Kuna siku tulipita tunakimbia hapa tuliposimama palikua ni dampo palikua hapatamaniki na kuna watu bado wanafanya biashara bila wasiwasi maana yake tumekosa ustaarabu.
 
“Nitoe  rai tunaomba mzingatie usafi na tutaweka sheria kali kidogo kwenye maeneo ya masoko kwa wale wote watakaokuwa wanatupa takataka.Kuna miji nchi hii ukienda ni misafi nenda Moshi tu hapo huwezi kuta mambo haya,” amesema Kihongosi.
 
Amesema wanataka kujenga hadhi ya jiji hilo ikiwemo kuzingatia usafi na kuwa wanahitaji jiji liwe safi hasa maeneo ya masoko kwani ndipo vyakula vinapouzwa na kuwa mazingira yasipokuwa masafi inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Awali akizungumza mara baada ya kumalizika kwa zoezi hilo la usafi sokoni hapo, Dk. Pima,amesema wajibu wa usafi ni wa kila mfanyabiashara katika eneo lake na kuwa wanataka kurejesha hadhi ya jiji hilo ikiwemo kuwa na mazingira safi.
 
“Wale mliokua hapa zamani mnafahamu watalii walikuwa wanafika mpaka sokoni hapa,tukiwa wachafu hakuna atakayesogea lakini hatutapata pia wateja wengi kwa hiyo jukumu la usafi tunataka liwe la kila mmoja kwenye eneo lake.
 
“Tumesikia changamoto ndani ya soko ikiwemo sehemu ya kutupa taka kule juu,tutakuja ili tuweke utaratibu na tutaleta moramu tuijaze kuna maji yanatiririka ndani ya soko tumepata neema ya mvua hivyo inakuja na mambo kama hayo,” amesema Dk. Pima.
 
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Chudaa Hassan, anasema soko hilo halina wamachinga na kuwa baadhi ya wafanyabiashara wenzao wameacha meza zao ndani na kwenda kuuza bidhaa zao nje ya soko.

Amesema kutokana na hali hiyo wao wanaofanya biashara ndani wamekuwa wakikosa wateja jambo linalowafanya wengine kushindwa kulipa mikopo ya mitaji yao.

“Nimefanya biashara kwenye hili soko miaka isiyopungua 20,kwa miaka mingi tumepata shida kwenye hili soko ya baadhi ya wenzetu kuacha meza zao ndani wakaja kufunga barabara,hatuuzi tunadaiwa ukituangalia sisi wote tunanuka madeni hatufai  tunafanya kukimbia kama panya.

“Tunaomba tusaidiwe hawa walioacha ofisi ndani wametoka nje na ikiwezekana mi naweza kujitolea kwa sababu ya wafanyabiashara wa ndani nikakutembeza meza ya kwanza mpaka ya mwisho nikikwambia hawa wamama wana vizimba ndani.

“Ukiangalia hakuna gari zinazopishana hapa, hakuna parking za biashara hata moja,tunalia kwa uchungu hatuna mahali pa kwenda,tunaomba utusaidie,” amesema.

Naye, Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika soko hilo, Fred Mollel,alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuomba uongozi wa halmashauri kusaidia kutatua changamoto hiyo.

“Ni kweli wamama wanalalamika ndani ya soko hawafanyi biashara,kuna tofauti ya barabarani na eneo la soko,waliotoka nje ndiyo wanafanya biashara kuliko waliopo ndani, tunaomba serikali itusaidi kuangalia hilo,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wamachinga mkoa wa Arusha, Amina Njoka, anasema wanapenda kushirikiana na serikali ikiwemo masuala ya usafi kwani lengo ni kila mtu awe na afya njema.

“Kuna baadhi ya watu wamepanga biashara zao barabarani nipo kazini nitapanga vizuri wapishe barabara ili kila mtu apite na afanye kazi kwa amani,wengine wanaweka siasa kwenye mambo ya msingi tunaomba tuondoleeni siasa huu ni muda wa kazi,kujijenga,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles