SHIRIKA Linalohusika na Sekta Mtambuka (BBIO) limetambulisha tuzo mpya iitwayo ‘Amani Awards’, inayolenga kufikisha ujumbe wenye dhamira inayobeba kazi mbalimbali za kimuziki, filamu na habari kwa ujumla.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Shirika hilo, Amani Mgullo, alisema lengo la kuanzisha tuzo hizo ni kuchangia dhima ya maisha bora na dunia bora kwa kila mwanadamu.
Alisema hiyo ni kuchochea umahiri katika kutoa, kueneza na kufikisha ujumbe wa maendeleo endelevu kupitia tasnia za muziki, filamu na habari.
“Tafiti zimethibitisha kuwa tasnia za muziki, filamu na vyombo vya habari vina uwezo mkubwa wa ushawishi na kufikia watu wote, matajiri kwa masikini, wake kwa waume, viongozi kwa waongozaji na zinavuka mipaka ya kimataifa,” alifafanua Mgullo.