22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

MAKAMU wa Rais ,Dk.Philip Mpango amemtaka Waziri wa Nchi, Muungano na Mazingira, Seleman Jafo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, kuandaa mpango mkakati wa kukijanisha na kusafisha Miji huku akitaka kupata taarifa za utekelezaji wa mpango huo kila baada ya miezi mitatu.

Makamu wa Rais, Dk.Philip Mpango akimpatia Nakala ya sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021,Mhariri wa Full Shangwe Blog, Alex Sonna Leo Februari 12,2022 Mara baada ya kuzindua sera hiyo.

Maagizo hayo ameyatoa leo Jumamosi Februari 12,2022,wakati wa uzinduzi wa sera ya Taifa ya mazingira ya mwaka 2021 ambapo Makamu huyo wa Rais amelitaka Jiji la Dodoma kuandaa mpango huo lengo likiwa ni kuifanya Dodoma iwe ya kijani.

“Mheshimiwa Waziri Jafo uniletee na  huo mpango mkakati na uwe wa kihalisia uniletee kila baada ya miezi mitatu sasa kwenye hili pale utekelezaji utakapotokea unalega lega natoa tahadhari wahusika wote wawajibike wenyewe kabla sijaingilia kati natumaini wamenisikia.

“Mfanye hivyo zoezi liwe endelevu na nataka niupate mpango huu ndani ya miezi mitatu tunataka Dodoma iwe kama Singapore lazima Dodoma iwe ya kijani lazima Dodoma iwe safi,” amesema Dk. Mpango.

Aidha, amewataka Mawaziri wa Kilimo, Maliasili na Utalii, Maji, Mifugo na Uvuvi pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwenda kufanya tathmini na kumpa majibu hatua walizochukua katika ujenzi wa  Bwawa la  mwalimu Nyerere.

Kwa upande wake, Waziri Jafo amesema awali kulikuwa na sera ya mwaka 1997 ambayo ilipata mafanikio makubwa na kuzalisha sheria  namba 20 ya mwaka 2004 na kanuni zake.

Amesema kwa kuwa sasa kwa sasa  kuna mahitaji makubwa na matakwa mbalimbali ilisababisha waunde  sera mpya ya mazingiraa ambayo imezinduliwa leo.

Amesema Juni 5, mwaka 2021, wakati Makamu wa Rais akizindua kampeni kapambe ya mazingira alitoa maelekezo ambayo ni pamoja na kuhakikisha sera ya mazingira inakamilika.

Amesema kwa kupitia sera hiyo Tanzania inaenda kuwa sehemu salama katika suala la mazingira na kuungana na mataifa mengine.

“Sera hii itaenda kuongeza fursa za jinsi gani urejeshaji wa taka unaweza kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja ama vikundi mbalimbali hili ni jambo ambalo lipo katika sera yetu jinsi gani tutatumia mbinu mbadala taka zinarejeshwa,”amesema Jafo.

Amesema sera hiyo  itaenda kuakisi hasa mabadiliko ya tabia nchi ambapo amemhakikishia Makamu wa Rais kwamba imezingatia   Mpango wa Taifa wa miaka mitano 2020-21mpaka 2025-2026 mpango endelevu wa mwaka  2030 na mpango ule wa  miaka 15 ulioanza mwaka  2011-2012 mpaka  2025-2026.

“Imani yetu mchakato wa sera hii utaenda kutekeleza masuala mbalimbali ambayo yataliokoa taifa letu hili na maelekezo yako ambayo umeyatoa muda wote kuhakikisha mazingira tunayatunza na tunayalinda kwa nguvu zote,”amesema.  

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Marry Maganga amesema maandalizi ya sera mpya ya mwaka 2021 yametokana na changamoto za uharibifu wa mazingira zilizosababishwa na mabadiliko ya kiuchumi zilizosabishwa na taka zinazozalishwa mijini na taka zitokanazo na vifaa vya umeme na viumbe vamizi.

“Mchakato wa maandalizi wa sera  ulihusisha wadau mbalimbali  napenda kuwashukuru ninawaomba muendelee na ushirikiano huu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema wamekubaliana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) kupanda  miti pembezoni mwa barabara ikiwemo katika ujenzi wa barabara za mzunguko wa nje katika Jiji la Dodoma.

Pia amesema wamekubaliana na Jiji la Dodoma kila mwenye kiwanja apande miti mitano mitatu ya matunda na miwili ya vivuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles