25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAENDELEO DUNI BARANI AFRIKA: Laana ya utawala mbovu na ufisadi uliokithiri

HILAL K. SUED

KWANINI Afrika, bara lililojaliwa na uwingi wa mali asili na ukubwa wa rasilimali-watu bado halijaweza kujiweka mahali pake stahiki katika madendeleo na siasa za dunia?

Miongoni mwa utajiri wa mali asili zake ni udongo wenye rutuba, mvua na jua la kutosha kwa ajili ya kilimo, mali ghafi nyingi, mafuta, gesi asilia na madini mengine tele. Lakini pamoja na haya ufisadi na utawala ndiyo hutajwa kuwa ni sababu za umasikini  na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Chukulia kwa mfano, mafuta yasiyosafishwa (crude oil) yanayozalishwa katika nchi kadhaa barani humu, ambayo yana ubora mkubwa na hivyo kuwa rahisi kuyasafisha.

Pamoja na hili wananchi wengi wa nchi hizo hawaoni manufaa yoyote kutoka kwa misururu wa wachimbaji na wawekezaji katika sekta hiyo. Mara nyingi wao (wananchi) ndiyo huumia kutokana na usafirishaji nje wa bidhaa hiyo na nyinginezo.

Inaelezwa kwamba kati ya 1970 na 1990 uchumi wa nchi zisizokuwa na utajiri wa mafuta zilikuwa kwa kasi ya mara tano kuliko zile zenye utajiri huo.

Mifano inayotajwa hapa ni nchi za Equatorial Guinea na Gabon, nchi mbili zilizo jirani zenye utajiri mkubwa wa mafuta lakini zinahesabiwa kuwa miongoni mwa mchi masikini duniani. Hali hii inahusishwa moja kwa moja na matumizi mabaya ya mali-asili hiyo yanayofanywa na uongozi wa kifisadi wakishirikiana na makampuni ya kibepari ya nje.

Nyingine ni Nigeria pamoja na utajiri wake mkubwa wa mafuta ambayo yamekuwa yanazalishwa na kusafirishwa nje tangu miaka ya 50. Miongo mingi ya ufisadi na utawala mbovu umesababisha umasikini mkubwa.

Katika maeneo ya jimbo la Rivers (Rivers State) ambako ndiko mafuta hayo huchimbwa wananchi masikini wamekuwa wakifa katika kupigania utajiri wao. Wamekuwa wakiyatoboa mabomba ya mafuta yanayopita katika maeneo yao ili kugida mafuta na kuyauza, mara nyingi husababisha milipuko na vifo.

Na hapa Tanzania inaelezwa kwamba mikataba mibovu na ya usiri mkubwa ya wawekezaji katika uchimbaji madini hususan dhahabu imeshindwa kupunguza umasikini miongoni mwa wamiliki halisi wa mali asili hiyo yaani wazalendo achilia mbali wale wanaoishi katika maeneo husika.

Hivi karibuni Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli amekuwa akijaribu kuona ni kiasi gani nchi ilikuwa inapunjwa na wawekezaji hao kupitia makontena ya mchanga yenye madini yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda nje kuchenjuliwa.

Hata hivyo inawezekana kwamba tunakumbuka shuka alfajiri kwani hali hiyo imekuwa ikiendelea kwa miaka 18 tangu utawala wa Awamu ya Tatu.

Hii inaonyesha kwamba kwa ujumla wananchi huwa hawana kauli ya mwisho katika kuchagua viongozi wanaowataka kusimamia mali asili zao, kwa sababu viongozi waliopo hutumia utajiri huo huo wanaoudhibiti katika kuendelea kukaa madarakani.

Lakini sasa hivi angalau kuna harakati za kuleta ahueni zinazojitokeza kuibadili hali hii, harakati zinazofanywa na makundi mawili katika jamii; vyombo vya habari na asasi za za kiraia.

Vyombo vya habari madhubuti na asasi za kiraia zenye bidii ni viungo muhimu katika kuleta demokrasia ya kweli yenye uwezo wa kupambana na ufisadi hata bila ya kujali nguvu kutoka kwa watu katika siasa.

Inaelezwa kwamba bila ya kuwepo vyombo vya habari vilivyo huru na asasi za kiraia makini, uwanja mkubwa hujitokeza kwa nguvu za siasa znazoshindikana kudhibitiwa ambazo matokeo yake ni ufisadi na tabia ya ukiukwaji wa demokrasia na maadili miongoni mwa wakubwa wa serikali.

Na juu ya hayo tawala mbalimbali zinazidisha mapambano yao dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na asasi za kiraia.

Wataalamu wa masuala ya ufisadi na utawala bora wanasema ufisadi hauna maana ya kuiba fedha za umma tu. Pia unahusu kuwaweka watu wasiofaa katika nyadhifa kubwa kubwa katika utawala – watu ambao hawana ari, uadilifu na sifa stahiki katika nafasi hizo. Aina hii ya ufisadi ndiyo hasa inaziathiri nchi nyingi barani Afrika kimaendeleo.

Kwa mfano ni kawaida katika idara au wizara ya serikali kukuta watendaji wengi kutoka sehemu moja ya nchi au hata kijiji kimoja, ambao wengi hawana sifa stahiki. Matokeo ya hali ya upendeleo wa namna hii kunaiathiri taasisi nzima na hata nchi kwa ujumla.

Hapo juu nimetaja kwamba ufisadi na kukosekana kwa utawala bora husababisha migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hali hii huwasukuma watu kuwa tayari kuzihama nchi zao kwenda kutafuta namna ya kuishi katika nchi nyingine ambako hufikiri kuna uwezekano wa kupata neema. Huwa hawafikiri kwamba nako huko kuna matatizo kama hayo wanayoyakimbia.

Kwa mfano, si mara moja au mbili kumezuka ghasia kubwa Afrika ya Kusini baina ya wazalendo wa huko na jamii za wageni pale wazalendo walipowashambulia wageni, hususan kutoka nchi zile za za jirani waliokwenda huko kutafuta kazi. Wazalendo walijikuta wanagombania ajira na wageni, kwani wao wenyewe ajira zilizopo hazitoshi.

Aidha hapa Tanzania tumeshuhudia katika miaka ya karibuni wimbi la wahamiaji haramu au ‘wapitaji haramu’ wanaopita kwenda kusini mwa Afrika kutafuta neema ya maisha.

Hawa wamekuwa wakikamatwa na mamlaka za uhamiaji na kufunguliwa mashitaka na hata kufungwa gerezani. Safari zao huwa za hatari sana kwani wengine hufa njiani katika makontena kwa kukosa hewa. Pamoja na hatari zote hizi, uhamiaji haramu wa namna hii haujakoma.

Katika moja ya makala zake za kila wiki katika magazeti kadhaa barani humu likiwemo la The African (liliokuwa gazeti dada la hili), Tajudeen Abdul-Raheem mwandishi wa Nigeria na mwanaharakati wa masuala ya Afrika aliyefariki mwaka 2009 aliwahi kuandika hivi: “Iwapo leo hii meli moja ya kigeni iliyoandikwa ubavuni “SLAVE SHIP” (yaani meli ya kubeba watumwa) itie nanga bandarini na watu kutangaziwa wajiandikishe katika vituo maalumu ili kuingia katika meli hiyo – misururu mirefu ya watu itaonekana katika vituo vya uandikishaji.”

Mwanzoni iliniwia vigumu sana kukubali iwapo kitu kama hicho (ujio wa meli ya namna hiyo) kitokee na uitikio wowote uwepo. Lakini baada ya kutafakari sana, niliona uitikio wa watu kujiandikisha kuingia katika meli hiyo unaweza kuwapo.

Bila shaka wengi wamekisoma kitabu kiitwacho “Roots” kilichoandikwa na Alex Haley, Mmarekani mwenye asili ya Afrika kinachoelezea historia ya biashara ya watumwa kutoka Afrika ya Magharibi na kupelekwa Marekani katika karne ya 18. Aidha kuna filamu iliyotengenezwa kutokana na masimulizi ya kitabu hicho.

Kitu kikubwa katika masimulizi hayo ni jinsi watumwa walivyokuwa wanasakwa, kukamatwa na kupakiwa katika meli bila ya kutaka kwao huku wakijihami kwa nguvu zao zote katika kila hatua ya biashara hiyo haramu. Kuna wengi walijirusha kutoka kwenye meli na kufa maji, kuliko kupelekwa wasikokujua.

Lakini ajabu ni kwamba katika karne hii na karibu miongo sita baada ya uhuru kinyume cha hayo ndiyo yanatokea – kuna watu kutoka Bara hili, kwa hiari yao wenyewe hujipakia katika vyombo hatarishi vya baharini kuelekea nchi za Ulaya na mara nyingi huzama na wao kufa maji, au kuishiwa chakula na maji na huwa ni bahati iwapo wataokolewa wakiwa hai.

Haya yametokea sana katika bahari ya Mediterranean kwa wahamiaji hususan kutoka Afrika ya Magharibi. Imekuwaje tena? Ni kutokana na hali ya kukata tamaa katika nchi mbalimbali barani humu, kama nilivyosema, hali inayotokana na tawala mbovu na ufisadi uliokithiri.

Na yote haya hufanyika chini ya kile kinachoitwa ‘demokrasia’ lakini kwa tafsiri ya sasa kinahusisha zaidi ukuaji wa nguvu za makampuni (corporate power) na propaganda zake zinazoenezwa kuilinda hali hii.

Siku hizi ‘demokrasia’ ni msamiati ambao watawala wengi kama wanalazimika kulitaja, basi hufanya hivyo kiunafiki kwani limekuwa ni neno lisilokuwa na maana yoyote.

Hii ni kwa sababu kila mtu, watu au vikundi vya watu hutoa tafsiri inayolenga kulinda masilahi yao na si masilahi ya waliyo wengi. Hawa hutulizwa kwa viambatanisho vyake – yaani propaganda zinazoenezwa kwa uwezo wao wa kifedha.

Na ndiyo sababu wananchi walio wengi hujikuta katika njia panda, bila msaada wowote na katika jitihada za kujikwamua, huamua kuchukua njia ya kuwakwepa wawakilishi waliochaguliwa ambao huwaona si chochote bali ni watu wa kati wanaowakilisha masilahi ya nguvu hizo za makampuni.

Miaka 18 iliyopita – ulipoanzishwa Umoja wa Afrika (AU) kama chombo mbadala cha iliyokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), kilibuniwa ndani yake chombo kingine kilicholenga kudhibiti hali hii – yaani kusisitiza utawala bora katika nchi za Kiafrika.

Jukumu kubwa la chombo hicho – African Peer Review Mechanism (APRM) lilikuwa ni kusisitiza nchi zijiratibu (self-monitoring) zenyewwe katika kuzishawishi kuwepo na usawa na maadili yanayopaswa katika masuala ya uchumi na ya siasa katika lengo zima la kuleta maendeleo ya uchumi na ya kijamii katika nchi za Afrika.

Hakika, sasa hivi ni vigumu kusema kuna mafanikio yoyote katika lengo lile. Tuchukulie siasa, kitu ambacho kama kinaendeshwa vyema kwa misingi inayokubalika ya kuwapa wananchi sauti ya kujiamulia mambo yao, ndicho kingewakwamua kutoka katika maendeleo yao duni.

Iwapo AU yenyewe, ambayo kwa kiasi fulani inao uwezo wa kuingilia masuala ya migogoro ya siasa ya nchi wanachama wake imeshindwa kumaliza migogoro katika nchi kadha, sembuse hili suala la kuzitaka nchi ziwe zinajiratibu zenyewe katika masuala ya utawala bora?

Katika kipindi tangu kuanzishwa kwa AU kumekuwapo mapinduzi ya kijeshi nchini Mauritania, Guinea, Ivory Coast, Madagascar, Mali, Zimbabwe na Burkina Faso. Pia kumekuwepo mapinduzi yaliyochochewa na umma katika nchi za Tunisia, Misri, Libya, Algeria na Sudan na bila kusahau machafuko ya kisiasa nchini Kenya, Ethiopia, Congo (DRC), Malawi, Burundi na Sudan ya Kusini. Na hapo hapo AU imeshindwa kumaliza mgogoro wa Somalia ulioachwa na OAU.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles