25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Baada ya al-Bashir nani atafuata?

OTHMAN MIRAJI

SIKU moja tu baada ya kupinduliwa kutoka madarakani Rais wa Sudan aliyekuwa madarakani, Omar al-Bashir, mkuu wa Baraza jipya la Kijeshi lililokamata madaraka nchini humo naye alijiuzulu.

Ijumaa iliyopita mkuu huyo- hapo kabla alikuwa waziri wa ulinzi- Awad Ibn Ouf, alimtaja Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kuwa mtu atakayekamata nafasi yake.

Punde baadaye mtawala huyo mpya alilihakikishia taifa kwamba haitachukua muda mrefu mamlaka yatakabidhiwa kwa raia. Jibula papo kwa papo; shangwe na vigelegele vya watu waliojaa furaha katika mabarabara ya mji mkuu wa Khartoum.

Utawala wa mabavu wa al-Bashir uliodumu miongo mitatu ulipinduliwa na jeshi alhamisi iliyopita baada ya kufanyika maandamano ya wananchi kwa mwezi mzima. Baraza la kijeshi liliundwa chini ya waziri wa ulinzi, Ibn Ouf, ili kuiongoza nchi hiyo katika kipindi cha mpito.

Pia mkuu aliyeongoza idara ya usalama ya Sudan alijiuzulu. Uongozi mpya wa nchi ulitangaza kwamba mkuu wa Baraza la Kijeshi amekubali kujiuzulu kwa Salih Ghosh.

Katika miezi iliyopita Ghosh aliitumia Idara ya Usalama wa Taifa kuyakandamiza kikatili maandamano ya wananchi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Madarze ni ya waandamanaji waliuliwa na maelfu ya wanaharakati, wapinzani na waandishi wahabari walikamatwa.

Mkuu mpya kijeshi pia alitangaza kuachwa huru wafungwa wa kisiasa ambao katika miezi iliyopota walikamatwa wakati wa maandamano. Katika hotuba yake kupitia televisheni siku ya jumamosi, Abdel Fattah al-Burhan aliahidi kwamba ataung’oa mfumo mzima wa utawalawa al-Bashir pamoja na mizizi yake.

Alitaja kwamba watu waliobeba dhamana ya kuuliwa waandamanaji itabidi wafikishwe mahakamani na kwamba amri ya watu kutotoka usiku nje ya majumba yao itaondoshwa.

Viongozi wa maandamano dhidi ya al-Bashir waliyakataa „Mapinduzi ya Kijeshi“ yaliyopikwa na wakatoa mwito wa kufanywa maandamano zaidi. Siku ya ijumaa maelfu ya watu walikusanyika mbele ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum wakitaka iwekwe madarakani serikali ya kiraia ya mpito. Baadaye ijumaa jioni Ibn Ouf alisema katika televisheni: “Natangaza hapa kwamba ninajiuzulu kuwa mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito“.

Pia makamo wake, Jenerali Kamal Abdelmarufu aliachishwa nyadhifa zake. Ibn Ouf alisema kwamba yeye ana imani na uongozi na uwezo wa mrithi wake kuiongoza jahazi hii na kuifikisha kwenye ufukwe kwa salama“.

Viongozi wa maandamano dhidi ya al-Bashir waliona kujiuzulu kwa Ibn Ouf kuwa ni ushindi kwa umma. Jumuiya ya wafanyakazi ambayo iliyaongoza maandamano ililitaka pia Baraza la kijeshi liyakabidhi madaraka haraka kwa serikali ya kiraia ya mpito, ama sivyo „mgomo wa watu kukaa mbele ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum na katika miji mingine utaendelea.

Muda mfupi kabla ya Ibn Ouf kujiuzulu, viongozi wa kijeshi waliahidi kwamba watakabidhi kwa haraka madaraka kwa serikali ya kiraia. „Haya si Mapinduzi ya Kijeshi“, alisema Jenerali Omar Zain al-Abidin alipokutana na mabalozi wa nchi za Kiarabu na Kiafrika. Jeshi „limesimama upande wa umma“.

Al-Abidin alitangaza pia kwamba jeshi litafanya mdahalo na vyama vya kisiasa juu ya kuundwa serikali ya kiraia. Kuhusu kuundwa serikali hiyo, Baraza la Kijeshi halitajiingiza.

Siku ya ijumaa, licha ya kutangazwa amri ya kuwakataza watu wasitoke nje usiku, maelfu ya watu walikusanyika mbele ya makao makuu ya jeshi. Muandamanaji aliliambia Shirika la Habari la Kifaransa, AFP, kwamba: „Damu ya wenzetu haijamwagika bure“. Kwa mujibu wa ripoti za polisi ni kwamba watu 16 waliuawa kwa kupigwa risasi kutokana na maandamano hayo na 20 wengine walijeruhiwa. Kamati ya Madaktari wa Sudan ilihakikisha idadi hiyo.

Ijumaa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kikao cha dharura lilijishughulisha na hali ya mambo ilivyo katika Sudan. Lakini baada ya kujadiliana kwa saa moja kikao hicho kiliacha kutoa taarifa. Balozi wa Kuwait katika Umoja wa Mataifa, Mansur al-Otaiba, alisema: hayo ni mambo ya ndani ya Sudan.

Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Jasir Abdesalam, alihakikisha mbele ya Baraza la Usalama kwamba Baraza jipya la Kijeshi nchini mwake,ilikuhakikisha usalama na amani,litakuwa mdhamini wa serikali ya kiraia. Alisema kwamba kipindi cha mpito cha miaka miwili kilichotangazwa kinaweza kufupishwa kufuatana na mambo yanavyokwenda.

Pia Baraza la Kijeshi liliziomba nchi jirani ziisaidie kifedha Sudan. Jenerali al-Abidin alisema Sudan inahitaji „michango“ ili kuyadhibiti matatizo ya kiuchumi ambayo yalipelekea kufanyika maandamano dhidi ya al-Bashir. Mafuta na ungani vitu vilivyo vichache katika nchi hiyo.

Mwaka 1989 al-Bashir kwa msaada wa watu wenye siasa za Kiislamu alifanya mapinduzi na akaingia madarakani. Tangu wakati huo amekuwa akiita wala nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Kwa miaka sasa kuna waranti uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ilioko The Hague, Uholanzi, inayotaka akamatwe kutokana na mauaji ya kimbari. Kwa mujibu wa habari za Umoja wa Mataifa katika Jimbo la Dafur, Sudan Magharibi, tangu mwaka 2003, wakati wa mzozo baina ya serikali kuu na waasi,watu 300000 waliuliwa. Watawala wapya huko Khartoum wamekataa kumkabidhi al-Bashir kwa mahakama hiyo ya The Hague.

Jumuiya ya Kupigania Haki za Binadamu Duniani, Amnesty International, imetaka al-Bashir afikishwe mbele ya mahakama hiyo ya kimataifa. Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Kumi Nadoo, alisema: mwishowe al-Bashir lazima aelezee juu ya makosa maovu kabisa dhidi ya haki za kibinadamu katika wakati wetu huu.

Kupinduliwa kwa al-Bashir kumepokelewa kwa kupumua na nchi mbalimbali za dunia, japokuwa wanajeshi wa huko Khartoum wametakiwa wairejeshe kwa haraka nchi yao katika utawala wa kiraia. Jumuiya ya Nchi za Ulaya imesema ni mwenendo wa kisiasa wenye kuaminika ndio utakaotoa haki kwa matarajio ya Wasudan.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani alisema wananchi wa Sudan wameweka wazi kwamba wanataka kipindi cha mpito kitakachoongozwa na raia.

Marekani bado inasita kufanya mazungumzo na Khartoum ambayo yataamua kama Sudan itolewe kwenye orodha ya nchi ambazo zinatuhumiwa kuunga mkono ugaidi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alitarajia kwamba juhudi za kidemokrasia za wananchi wa Sudan kupitia serikali ya mpito, zitafanikiwa. Aliwataka Wasudan watakaoshiriki katika mwenendo huo wachunge „utulivu na wawe wenye subira“.

Angalau sasa amepungua mtawala mmoja mwingine wa kidikteta barani Afrika, japokuwa haijulikani nani hasa atamfuata al-Bashir huko Sudan. Lakini jambo moja ni wazi, nalo ni kwamba Wasudan,kama walivyofanya majirani zao-Waalgeria- wiki chache zilizopita walipompindua kutoka madarakani Rais Abdelazizi Bouteflika-wamedhihirisha kwa mara nyingine tena kwamba hamna nguvu zozote zinazoweza kuzuia nguvu kubwa na hamu ya wananchi kutaka kuleta mabadiliko na kuzishinda nguvu za dhuluma na zinazotaka kuwanyima haki zao za kimsingi, kama vile uhuru, demokrasia na maisha yaliyo bora.

Ni dikteta gani mwingine atakayefuata hatuwezi kutabiri.

Mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles