28.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

WASANII WASAIDIWE KUZIFIKIA DILI ZA KIMATAIFA

NA CHRISTOPHER MSEKENA


WAKATI tukishuhudia wasanii wachache wasiopungua watatu kutoka Tanzania wakipata nafasi ya kushiriki katika dili za kimataifa, tunapaswa kutafakari namna nyingine sahihi ya kuongeza idadi hiyo.

Wasanii kama Cassper Nyovest kutoka Afrika Kusini, wamekuwa kwenye orodha ya wasanii wakubwa barani Afrika ambao wanapata dili nono za kimataifa zinazomwingizia kipato kikubwa nje ya kazi yake ya muziki.

Wiki chache zilizopita rapa huyo alipata dili la ubalozi wa kinywaji cha Ciroc, ambacho kinamilikiwa na Sean Combs ‘P Diddy’ wa Marekani, huku akiwa mlipaji mzuri wa kodi kwa kila dili analopata.

Hapa Bongo bado hali ni tete, wasanii wanalazimika kutumia nguvu zao binafsi kutafuta kolabo  za kimataifa, ambazo tunatarajia ziwakutanishe na kampuni kubwa zitakazowapa dili, ila wanakutana na vikwazo vingi sana vinavyowarudisha nyuma.

Binafsi natamani kuona Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiweka hadharani mikakati yake ya kuhakikisha kwa mwaka wasanii kadhaa wapate dili kubwa za kibalozi kutoka kampuni za kimataifa.

Natamani kuona Wizara yetu inakuwa mstari wa mbele kuwaunganisha wasanii wetu na wale wa kimataifa ambao ni ngumu kuwapata kwa njia binafsi, ili wafanye nao kazi, lengo likiwa ni kutanua muziki wetu.

Kwa sababu msanii anapofanikiwa hulipa kodi, anatengeneza ajira kwa vijana wengine na kufanya kiwanda cha burudani kikue kwa kasi, hasa kipindi hiki kuelekea Tanzania mpya ya viwanda.

Tunaona Diamond anavyojitahidi kuonyesha namna msanii akisimamiwa vizuri anavyoweza kuwa na tija kwenye nchi. Tunapofurahia mafanikio ya Ali Kiba kuja na bidhaa yake ya kinywaji, basi tufikirie kuwatengenezea mazingira rafiki wasanii wengine.

Na njia ni moja tu ya kuwapa ushirikiano na uhuru wa kufanya kazi zao bila kuwawekea mipaka. Sitaki kuamini kama tatizo ni hili moja tu la wasanii kuvunja maadili ambalo limekuwa likipigiwa kelele zaidi.

Kuna matatizo lukuki ambayo yanawakwamisha wasanii kibiashara kwenye anga la kimataifa kama wanavyopata wasanii wa mataifa mengine. Tutatue matatizo hayo tukimaliza hili la maadili na wahusika wawe mstari wa mbele kutengeneza njia za wasanii wetu kutazamwa kwa jicho la kibiashara na mataifa mengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles