MASTAA WAUNGANA KUMUOMBEA MSAMAHA MAUA SAMA

0
2606

Na SWAGGAZ RIPOTA


HUENDA hili likawa fundisho kwa  jamii kuipa heshima fedha yetu kwa kutoifanyia dhihaka yoyote kwa kujua au kutokujua baada ya tukio la mkali wa Bongo Fleva, Maua Sama na mtangazaji Soud Brown kukamatwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Hatua ya Maua Sama na Soudy Brown kutiwa nguvuni ni baada ya kuchapisha video ya watu wanaochezea, kuzitupa na kukanyaga noti za shilingi 10,000 wakiwa wanaucheza wimbo Iokote.

Gumzo limekuwa kubwa katika mitandao ya kijamii na vilinge vingine vya burudani baada ya udhibitisho kutoka kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliyeliambia Swaggaz kuwa wawili hao wanashikiliwa kwa kutenda kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu namba 332A  cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai (Penal Code) sura ya 16 kama ilivyorejewa mwaka 2002.

Hata hivyo baada ya mastaa hao kukamatwa, wasanii mbalimbali nchini wameonyesha hisia zao kutokana na tukio hilo, huku wengine wakiwaombea msamaha kwa maelezo kuwa wanaamini hawakukusudia.

Wakieleza hisia zao wakati wakiwaombea msamaha mastaa hao, wasanii hao wameomba Jeshi la Polisi liwape nafasi ya kujirekebisha ili wawe mabalozi na mfano kwa vijana wengine wasiige kosa kama lao.

Swaggaz linaungana na mastaa hawa wafuatao ambao wamepaza sauti zao kuwaombea msamaha Maua Sama na Soudy Brown kutokana na kosa hilo lililowaweka nyuma ya nondo kwa siku saba sasa.

 

VANESSA MDEE

Staa huyu wa muziki ambaye hivi sasa yupo nchini Ujerumani kwa shughuli zake za muziki, amempa pole Maua Sama kwa msukusuko huo huku akimtuma mdogo wake Mimi Mars kwenda kituoni kumjulia hali.

“Najua utakuwa umelia mpaka, lakini hivi karibuni utatoka na tutacheka tena na kuhadithiana stori za humo ndani, Mungu anakupenda sana na ushuhuda wako utamuaibisha sana adui,” aliandika Instagram.

 

IDRIS SULTAN

Huyu alikuwa wa kwaza kupata sauti za kumuombea amsamaha Maua Sama kwani anaaamini mrembo huyo anaweza kutumika kwa ushawishi alionao kama balozi wa kuielimisha jamii juu ya utunzaji wa fedha za Tanzania.

“Ningependa kupendekeza mumtumie Maua kuelimisha wengine kupitia ushawishi wake, na adhabu aliyopata mpaka sasa tufanye imetosha, hakuna aliye juu ya sheria ila tuvae tu uhusika wa lengo,” alisema Idris.

 

STEVE NYERERE

Katika sakata hili la maua Sama na Soudy Brown, Nyerere amejitokeza na kuliambia Swaggaz: “Haipendezi mtu kuchezea fedha wakati wengine wana shida, kuna watu wanahangaika kutafuta 1000 tu ya matibabu, mwingine anahangaika kutafuta ada, kodi nk, kwa hiyo pesa haipaswi kuchezewa ila hili kwa niaba ya wasanii wenzangu tunaomba radhi, tunaomba wapate dhamana kwani naamini walifanya hivyo kwa sababu walikuwa hawajui kuwa ni kosa.”

 

GIGY MONEY

Gift Stanford maarufu Gigy Money ambaye ni rafiki wa karibu na Soud Brown na Maua Sama,  yeye amesema: “Kila kitu kinachotokea kinakuwa na sababu ya kumkuza mtu na kumfundisha kwa hiyo namuomba Maua amwamini Mungu hili litapita.”

 

SHILOLE

Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ambaye ni msanii wa muziki na mjasiliamali naye amewapa pole Maua Sama na Soudy Brown kwa kuwa kwenye matatizo hayo.

Kupitia ukurasa wake wa picha Shilole alisema: “ Hili nalo litapita Inshaaalllah ndugu zangu, Watanzania tuwaombee huko walipo.”

 

BARNABA

Elius Barnabas ambaye ni staa wa Bongo Fleva amesema: “Naamini mkono wake nawaombea heri na baraka ukawaguse, najua Watanzania wengi wanawahitaji na mmekuwa watu wa mfano wa vijana wengi.  Nachukua jukumu hili kuwaombea kwa Mungu na naamini yatapita mitihani ni sehemu ya maisha.”

 

WOLPER

Jacquline Wolper ambaye ni msanii wa filamu na mbunifu wa mavazi amewaombea msamaha Maua na Soudy Brown kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Yeye ameandika: “Katika utafutaji kuna mitihani mingi, ninachoweza kusema ni kuomba tu wakubwa muwasamehe vijana wenzetu. Naamini katika hili lililotokea basi wengine wengi watajifunza kitu kupitia hili. Naomba niwaombee masamaha wa dhati kabisa ndugu zetu na wawe huru kuendelea na majukumu yao.”

 

DIAMOND, RAYVANNY WATAJWA

Katika hatua nyingine, wasanii Diamond Platnumz na Rayvanny wametajwa katika mijadala mbalimbali inayohusu sakata hili kutokana na tangazo lao la bidhaa za karanga linaloonyesha wanafanya kile ambacho kilionekana katika video iliyowatia matatani Maua Sama na wenzake.

@@@

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here