MWILI wa binadamu na viumbe wengine kama vile wanyama, una mfumo unaosaidia kujilinda dhidi ya magonjwa mbalimbali. Mfumo huu wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa kwa kitaalamu huitwa ‘Immune system.’
Pamoja na mwili kuwa na mfumo wa kujilinda dhidi ya magonjwa, kuna nyakati ambazo kinga hii ya mwili inakuwa haijakomaa mfano kwa watoto. Pia kutokana na tafiti mbalimbali za kitabibu juu ya afya na uwezo wa mwili kujilinda, imesababisha kuwapo umuhimu wa kuimarisha kinga ya mwili kupitia matumizi ya chembe chembe ambazo hujulikana kwa jina la chanjo au kwa kitaalamu ‘Vaccine.’
Chanjo au ‘Vaccine’ ni chembechembe ambazo huandaliwa kupitia viumbe au bakteria wasababishao magonjwa (microbes), au chembechebe zinazoandaliwa kwa kutengenezwa (synthetic) ili kutumika katika kuuandaa mwili au kuamsha kinga ya mwili iweze kupambana na ugonjwa au magonjwa mbalimbali.
Kutokana na aina ya matumizi, chanjo zimegawanyika katika makundi makuu mawili. Makundi hayo ni chanjo itokanayo na bakteria au virus ambao wameondolewa uwezo wao wa kusababisha ugonjwa (An attenuated vaccine) na kundi lingine ni chanjo ambayo hutokana na bakteria au virus ambao tayari wameuliwa/hawana uhai (Inactivated vaccines).
Miongoni wa chanjo ambazo zimekuwa zikitolewa kwa binadamu ni pamoja na chanzo dhidi ya magonjwa kama vile surua, tetenasi, polio, homa ya ini (Hepatitis A and B) pamoja na chanjo ambayo imezinduliwa hivi karibuni nchini, Tanzania, chanjo ya kumkinga mwanamke dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi (Human papilloma virus (HPV) vaccine).
Chanjo imekuwa na umuhimu mkubwa katika mnyororo wa tiba za magonjwa mbalimbali. Baada ya kinga ya mwili kuamshwa na kuimarishwa, athari za magonjwa mbalimbali kwa binadamu zimekuwa zikipungua, mfano ulemavu (kupooza kwa viungo), magonjwa ya ini na vifo vimepungua.
Sababu kubwa ya matumizi ya chanjo au utoaji wa chanjo ni kufanya mwili uweze kuzalisha kinga dhidi ya ugonjwa husika (Specific antibodies to each individual disease).
Â
Je, chanjo hutolewa kwa kundi lipi la watu?
Kama ambavyo nimetangulia kwa kufafanua maana ya chanjo, kuwa ni chembechembe ambazo zinatokana na aina ya viumbe au bakteria wanaosababisha magonjwa, kuna tahadhari katika makundi ya watu ambao watakuwa na sifa ya kupatiwa chanjo husika.
Kwa mtu ambaye tayari analo tatizo husika, mfano mtu mwenye tatizo la homa ya ini (Hepatitis A au B), hatopatiwa chanjo ya ugonjwa huo, kadhalika na magonjwa mengine. Si salama kumpatia mtu chanjo wakati tayari analo tatizo au ugonjwa husika. Kumpatia mtu chanjo huku akiwa na tatizo au ugonjwa husika, kunaweza kusababisha tatizo likawa kubwa zaidi hatimaye kuhatarisha afya na uhai wa mgonjwa. Pia, chanjo zimekuwa zikitolewa kulingana na umri wa mlengwa/mteja.
Baada ya chanjo kutolewa, kwa baadhi ya nyakati pia zimekuwa zikisababisha maudhi madogo madogo kwa mtumiaji. Mfano kwa watoto wadogo zimekuwa zikisababisha joto kupanda, usumbufu katika kusikia, maumivu sehemu iliyo chanjwa mfano sehemu ya mkono au paja.
Maudhi haya madogo madogo siku zote yamekuwa si lengo kuu la chanjo, bali hujitokeza kwa baadhi ya watu. Matibabu ya maudhi haya yanategemeana na aina ya usumbufu ambao umejitokeza kwa mtu, si matibabu ya jumla kwa watu wote.
Miongoni mwa matibabu au msaada wa kitabibu ambao umekuwa ukitolewa kwa watu ambao wamepatwa na matatizo baada ya kupatiwa chanjo ni pamoja na matumizi ya dawa za kushusha joto au homa, dawa za kuondoa degedege (convulsions) pamoja na matibabu mengine kutegemeana na namna ambavyo yamejitokeza.
Ili kuepukana na magonjwa mbalimbali pamoja na athari zake kiafya na kijamii, ni vyema walengwa wote wakapatiwa chanjo kulingana na miongozo inayotolewa na wataalamu wa afya.