Na Editha Karlo, Kigoma
TANZANIA ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa na ugonjwa wa malaria.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linautaja ugonjwa huu kuwa ni hatari, unaosababisha vifo vya watu wengi duniani. Miongoni mwa watu wanaoathirika zaidi  ni akina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Ndiyo maana wataalamu wa masuala ya afya wanasisitiza kuwa kila mtu anatakiwa kuchukua tahadhari ili kupunguza idadi ya vifo vinavyoweza kuzuilika kwa kuafuata kanuni za afya na maelekezo ya kitabibu, kama yanavyotolewa na watoa huduma ya afya.
Ili kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa la mfano katika kupambana na adui malaria, wataalam wa afya wanaendelea kutafuta ufumbuzi wa kuona ni jinsi gani wanapunguza au kumaliza kabisa tatizo hili linalomaliza nguvu kazi ya Taifa nchini.
Aprili 25 mwaka huu, mataifa yote duniani yaliadhimisha Siku ya Malaria Duniani, ambapo kwa hapa nchini yalifanyika mkoani Kigoma, Wilaya ya Kasulu, yakiongozwa na kauli mbiu ya ‘Nipo Tayari Kutokomeza Malaria Wewe Je?’
Katika maadhimisho hayo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alizindua ripoti ya matokeo ya utafiti wa viashiria vya malaria kwa mwaka 2017.
Akizindua ripoti hiyo, anasema takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha malaria kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kimeshuka hapa nchini kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 7.3 mwaka jana. Hii ni  kwa kutumia kipimo cha haraka cha utambuzi wa vimelea (mRDT).
Anasema utafiti huo unaonyesha mikoa yenye kiwango kikubwa cha watoto wanaogua ugonjwa wa malaria, kiwango kwa asilimia kwenye mabano, ni Kigoma (asilimia 24.4), Geita (asilimia 17.3), Kagera (asilimia 15.4) na Tabora (asilimia 14.8).
Wakati mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Njombe, Songwe na Dodoma ikiwa na kiwango kidogo cha maambukizi, chini ya asilimia moja.
“Takwimu hizi zinaonyesha ni jinsi gani malaria imepungua kwa kiasi kikubwa. Hii ni habari njema kwetu sote, inaonyesha ni jinsi gani serikali yetu inatoa kipaumbele kudhibibiti malaria hatimaye kuitokomeza kabisa,” anasema Ummy.
Anasema ili Serikali ifikie malengo ya kutokomeza ugonjwa wa malaria, jamii inapaswa kufanya kazi kwa pamoja kwani watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wajawazito ndio waathirika wakubwa.
Anasema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kutokomeza ugonjwa huu, zipo changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi ili kuweza kufikia malengo.
Ummy anazitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na wanajamii kutotumia vyandarua ipasavyo, kuwapo kwa mitazamo potofu juu ya hatua za kupambana na malaria, mfano dhana ya viuatilifu ukoko za kunyunyuzia dawa ukutani, kwamba zinaleta kunguni na viroboto ndani, huku vyandarua vikidhaniwa kupunguza nguvu za kiume.
Anasema jamii haishiriki kikamilifu katika kutunza mazingira na kuharibu mazalia ya mbu kwa kuondoa maji yaliyotuama.
“Acheni kusikiliza mambo ambayo hayana ukweli wowote, Tanzania bila malaria inawezekana kabisa,” anasema.
Anasema ili kupunguza au kuondoa kabisa changamoto zilizopo, wizara inaendelea kutekeleza ipasavyo mikakati muhimu ya kupambana na ugonjwa wa malaria kama inavyopendekezwa na WHO.
“Licha ya kufanikiwa kwa asilimia kubwa kupunguza ugonjwa huu, wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa malaria ni hatari kwa uhai na maendeleo ya ustawi wa Taifa letu,” anasema.
Ummy anawataka wananchi kuhakikisha wanalala kwenye vyandarua vyenye viuatilifu kila siku, na kwamba kila mtu mwenye dalili za malaria ahakikishe anawahi kwenye kituo cha kutolea huduma za afya ili aweze kupata vipimo na akikutwa na vimelea basi atumie dawa kulingana na maelekezo ya daktari.
Aidha, anasema wajawazito wote wahakikishe wanahudhuria kliniki mapema ili waweze kupata huduma zote muhimu ikiwamo kupata kinga ya tahadhari (SP).
“Sasa hivi tumeongeza kasi ya upimaji ili kuhakikisha wagonjwa wanaodhaniwa kuwa na malaria wanapimwa kwa kutumia kipimo kinachotoa majibu haraka (mRDT),” anasema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk. Albina Chuwa anasema lengo kuu la utafiti wa viashiria vya malaria kwa mwaka 2017 ni kutoa taarifa za kiwango cha malaria na upungufu wa damu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Anataja malengo mengine kuwa ni kutoa taarifa kuhusiana na hali ya makazi, umiliki, upatikanaji na matumizi ya vyandarua na upatikanaji wa huduma ya kinga dhidi ya malaria kwa wajawazito. Kwa hiyo, takwimu hizo zitatumika kufuatilia na kutathmini malengo yaliyowekwa katika mpango wa pili wa maendeleo ya Taifa.
“Hili la takwimu naomba nilisema kama mtaalamu na si mwanasiasa, ukiangalia hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka jana, umeendelea kukua kwa asilimia 7.1 ukilinganisha na asilimia 7.0 mwaka 2016. Hapo ukitafsiri haraka ni kwamba baadhi ya shughuli za uchumi kama vile za afya na huduma za jamii zimechangia katika ukuaji huo,” anasema.
Dk. Chuwa anasema katika kipindi cha mwaka jana, shughuli za kiuchumi za afya na huduma za kijamii zinaendelea kukua kutoka asilimia 5.2 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 5.9 mwaka 2017. Hivyo, afya ya huduma za kijamii zinaendelea kuimarika zaidi na kufanya kuimarisha uchumi wa nchi.
“Nafahamu wapo watakaobeza juhudi hizi, lakini ukweli utabakia kuwa huo huo wa ongezeko la asimilia 0.7 katika ukuaji wa uchumi kwenye sekta ya afya na huduma za jamii ni pamoja na juhudi zinazofanywa katika sekta ya afya kwa serekali yetu,” anasema.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Marekani, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), Andy Karas, anasema mpango wa Rais wa Marekani wa Malaria (PMI), unajaribu kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huu, pia kupunguza kuenea kwa malaria ikiwa ni pamoja na kuweka malengo ya kutokomeza ugonjwa huo.
Anasema PMI kwa upande wa Tanzania Bara, wameweza kunyunyuzia dawa za kuua mbu katika nyumba 575,000, wamegawa vyandarua vyenye dawa zaidi ya 900,000 kwa watoto wa shule za msingi katika mikoa minne yenye kiwango kikubwa cha ugonjwa wa malaria.
Pia wameweza kuzindua mpango wa kutoa vyandarua bure kwa wajawazito wanaohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza na watoto wanaopatiwa chanjo ya kwanza.
Anasema kuna changamoto kadhaa wanazokumbana nazo katika kudhibiti ugonjwa huu, ambazo ni uhaba wa rasilimali watu, ukosefu wa maafisa wa malaria wenye ujuzi, uhaba wa wafanyakazi, usimamizi duni wa mfumo wa ugavi wa afya na ugumu wa utoaji wa huduma za tiba na kinga katika vituo vya afya nchi nzima.
Mkurugenzi huyo anasema kuwa PMI inasaidia kuongeza nguvu katika jitihada za USAID ili kuimarisha mifumo ya afya na kuweza kutatua changamoto hizo.