CARACAS, VENEZUELA
KIONGOZI wa upinzani wa Venezuela aliyejitangaza rais wa mpito, Juan Guaido, ameitisha maandamano ya amani kwenye vituo vya kijeshi vya nchi hiyo, siku chache baada ya jaribio la uasi wa wanajeshi wanaomuunga mkono kushindwa.
Wito huo unakuja muda mfupi baada ya Rais Nicolas Maduro, kulitaka jeshi kuzima dalili yoyote ya mapinduzi dhidi ya Serikali yake. Kwenye ujumbe wake wa Twitter, Guaido amewataka wafuasi wake kukusanyika kwa amani leo Jumamosi kwenye makambi ya kijeshi ili kuwashinikiza wanajeshi kuunga mkono katiba.
Wiki iliyopita, kiongozi huyo anayetambuliwa na zaidi ya mataifa 50 duniani kama rais wa mpito wa Venezuela, alitoa wito kwa wanajeshi kuungana naye kumwondoa Maduro na kundi dogo la wanajeshi likajitokeza kumuunga mkono. Lakini punde vuguvugu hilo lilizimwa na kuchochea siku mbili za maandamano ya ghasia mitaani, ambapo watu wawili waliuawa.