CALIFONIA, MAREKANI
WAKATI watumiaji wa mtandao wa Zoom wakiongezeka kutoka milioni 10 kwa siku hadi milioni 200, Kanisa moja huko Califonia linashtaki kampuni hiyo baada ya mvamizi mmoja kuvamia darasa la mafundisho ya bibilia yaliokuwa yanaendelea mtandaoni na kutuma picha za unyanyasaji wa watoto kingono.
Mvamizi huyo alivamia mkutano huo na kuchezesha picha za video zenye kutatiza akili”, kulingana na kesi iliyowasilishwa na Kanisa la Lutherani la Saint Paulus.
Viongozi wa kanisa la San Francisco waliwasiliana na kampuni ya Zoom kutafuta usaidizi lakini kampuni hiyo haikuchukua hatua yoyote.
Katika taarifa, msemaji wa kampuni ya Zoom ameshtumu tukio hilo baya na la kiovu.
“Tunahuzunika pamoja na wale walioathirika,”kampuni hiyo imesema, “Siku hiyo hiyo tulipogundua tatizo hili, tulimtambua aliyetekeleza kitendo hicho, tukachukua hatua kwa kumfungia asiweze kuingia kwenye mtandao wetu na kuwasilisha taarifa kwa mamlaka husika.”
Kampuni hiyo imezungumzia hatua za kiusalama walizochukua hivi karibuni katika mtandao wao”, na kuongeza kwamba watumiaji wa kampuni ya Zoom hawastahili kushirikisha watu wengi sana namba zao za siri za kuwawezesha kufanya mkutano kama ilivyoonekana kwa kundi hilo la kanisa.
Umaarufu wa mikutano kwa njia ya video kupitia mtandao wa Zoom umeongezeka sana katika miezi ya hivi karibuni hasa kwa wafanyakazi na hata kwa shughuli za kibinafsi wakati ambapo nchi kadhaa zimechukua hatua ya kusalia ndani kama njia ya kukabiliana na virusi vya corona.
Utumiaji mkubwa wa mtandao huo wa zoom umekumbwa na mashaka ya kiusalama na faragha ya watu, ambapo wavamizi wamekuwa wakivamia mikutano ya watu bila kualikwa na wakati mwingine wakituma ujumbe wa chuki, kibaguzi, unyanyasaji au hata picha za ngono.
Kanisa la Saint Paulus – moja ya makanisa ya zamani huko San Francisco – limesema kwamba kesi hiyo iliyowasilishwa katika mahakama moja iliyopo San Jose Jumatano, inalalamikia tukio la Mei 6 wakati wa mafundisho ya bibilia ambayo yalivamiwa na mtu aliyefahamika – ambaye pia ameripotiwa kwa mamlaka mara kadhaa.
Wanafunzi wanane wanaojifunza mafundisho ya bibilia, wengi wao wakiwa wale wanaopokea malipo ya uzeeni, mfumo wao wa kompyuta ulikatishwa wakati mvamizi huyo alipocheza video za ngono.
Wakati ambapo programu ya zoom imeendelea kupata umaarufu, imekumbwa na ukosoaji mkubwa kwasababu za kiusalama.
“Video hizo zilikuwa mbaya na ilikera zaidi kuonesha watu wakubwa wakijihusisha na vitendo vya ngono miongoni mwao, kufanya vitendo vya ngono dhidi ya watoto na wale wachanga, pamoja na kuwanyanyasa kimwili,” kesi hiyo inasema
Wakati wanafunzi hao walipojaribu kufunga video hiyo na kuanza tena, mvamizi huyo alivamia tena, kesi hiyo inaongezea.
Kanisa hilo limewasilisha mashtaka likitaka hatua kuchukuliwa dhidi ya kampuni ya Zoom yenye makao yake San Jose.
Katika kesi hiyo, waliowasilisha mashtaka wanataka kufidiwa kwa madai ya kupuuzwa, kukiukwa kwa mkataba, ukosefu wa haki na tabia zisizofaa katika biashara.
Kampuni ya Zoom iliandika kwenye blogu kwamba imechukua hatua zaidi za kiusalama wiki hii na kuahidi hatua za kuimarishaji usalama ikiwemo mipango ya kumzuia mtu wa kando kuingilia mawasiliano ya mtumiaji.
Awali, kampuni hiyo ilikosolewa kwa kudai kwamba tayari hatua za kumzuia mtu wa kando kuingilia data ya mtumiaji zipo kumaanisha kuwa ni mtumiaji pekee anayeweza kufikia ujumbe wake na video zake.
Kile kilichoikumba kanisa hilo ndicho kilichotokea katika kikao cha bunge cha Afrika Kusini wiki moja iliyopita.
Mkutano wa kamati ya bunge kwa njia ya mtandao Afrika Kusini uliwahi kuvamiwa na wadukuzi na spika kudhalilishwa.
Kikao hicho kilikuwa tu ndio kimeanza picha za ngono zilipojitokeza kwenye skrini huku sauti ya mwanamume ikisikika kumtusi Spika Thandi Modise, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho.
Spika huyo aliyeshikwa na hasira alipaza sauti akisema hiyo ndio sababu anapinga mikutano ya mitandaoni.
“Hiki kilichotokea ni kilekile nilichokuwa ninakisema kuhusu kufanya mikutano kwa njia ya Zoom!” Modise amenukuliwa akisema hivyo na tovuti ya Times Live.
Wabunge walielezea tukio hilo kama lenye kukera na kutatiza akili, kulingana na Tovuti ya habari ya Eyewitness.
Iliwalazimu wahandisi wa Bunge kutuma kiunganishi kingine ambapo wabunge waliungana tena na kuendelea na kikao chao.
Kampuni ya mtandao wa Zoom imekuwa ikikosolewa kimataifa kwa taarifa kwamba kuna wavamizi wanaotuma picha za ngono au maudhui ya matusi wakati wa mikutano.
Kuvamiwa kwa mtandao kwa njia ya Zoom kumekuwa kukifanyika mara kwa mara katika wiki za hivi karibuni wakati ambapo watumiaji wengi wapya wameanza kutumia mtandao huo kama njia moja ya kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa wa Covid-19 na kuahirishwa kwa mikutano na matukio ambayo awali ilikuwa ifanyike ana kwa ana.